Siasa

Utafiti: Gen Z wako tayari kuamua 2027

Na NDUBI MOTURI na WACHIRA MWANGI November 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

WAPIGA kura wa kizazi cha Gen Z wameashiria mabadiliko makubwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao kwa kusema wako tayari kushiriki.

Hata hivyo, wasiwasi unaibuka kwa kuwa hawajitokezi kujisajili kama wapiga kura.

Utafiti mpya uliofanywa na kampuni ya utafiti ya Odipo Dev ili kuchunguza hisia za vijana baada ya maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha, unaonyesha kuwa karibu vijana saba kati ya kumi wanakusudia kupiga kura katika uchaguzi ujao, kiwango ambacho hakijashuhudiwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

Hata hivyo, utafiti huo unatahadharisha kuwa usajili wa wapiga kura ndio kikwazo kikuu, huku imani duni kwa mfumo wa uchaguzi ikidhoofisha misingi ya nguvu mpya za kisiasa miongoni mwa vijana.

“Kuna kutoamini sana Tume ya IEBC kulingana na mahojiano tuliyofanya. Wanaamini kuwa kuna ushawishi mkubwa wa kisiasa na kwamba kura zao hazitahesabiwa katika uchaguzi ujao. Hii imewazuia wengi kujisajili,” anasema Bi Winny Jerotich, mtafiti wa vijana na vyombo vya habari wa Odipo Dev.

Utafiti huo ulilenga kuelewa kile unachoita “ndoto ya kisiasa ya Gen Z”, mtazamo wa siasa mpya, uwajibikaji wa kweli na serikali inavyotekeleza wajibu wake.

Lakini utafiti uligundua kuwa kizazi hiki kilichozinduka kisiasa kinakwamishwa na mchakato wa uchaguzi ambao hakiuamini.

Watafiti wanaeleza hali hiyo kama “viwango vya juu vya kukosa uaminifu katika uchaguzi,” mtazamo unaopunguza idadi ya wanaojitokeza kupiga kura na kuzuia vijana wengi kujisajili.

“Baada ya maandamano ya 2024, Gen Z wameonyesha kuongezeka kwa uwajibikaji wa kiraia na nia ya dhati ya kupiga kura, lakini usajili duni ndio kikwazo kikubwa zaidi. Swali pana zaidi ni jinsi ya kuwaekeleza vijana hawa kwenye safari hii,” ripoti inaeleza.

Utafiti unaonyesha pia mabadiliko katika sababu zinazoathiri kupungua kwa ushiriki wa vijana katika siasa. Kabla ya 2025, kutoshiriki kwao kulitokana na hisia za kukata tamaa, kutoamini mfumo wa uchaguzi, kukerwa na viongozi wasiotimiza ahadi na kutoona mabadiliko kupitia kura.

Mwaka huu, sababu hizo zimekuwa ngumu zaidi. Mbali na kutoamini mfumo wa uchaguzi, vijana sasa wanasema wamechoshwa na ahadi hewa za kampeni, taasisi zisizo wazi na hisia kwamba wagombeaji wengi ni ‘ wale wale katika rangi tofauti.’ Ripoti inataja hili kama mabadiliko kutoka kukata tamaa kimya kimya hadi wasiwasi kutokana na ufahamu zaidi, ishara kwamba mabadiliko yanahitajika lakini bado wakiwa na shaka iwapo mfumo wa uchaguzi unaweza kuyaleta.

Utafiti unadokeza kuwa 2027 huenda ukawa mwaka wenye idadi kubwa zaidi ya vijana kupiga kura tangu 2013, iwapo usajili utaimarishwa. Pia, unaonyesha mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa taarifa: mitandao ya kijamii inaongoza, lakini zana za Akili Unde (AI) zinaibuka kwa kasi.

Kwa mujibu wa utafiti, asilimia 37 ya vijana wa miaka 18–19 wametumia zana za AI kutafuta taarifa za wagombeaji katika chaguzi ndogo.

Mazungumzo na marafiki na watu wanaowaamini bado ndiyo huwafanya kuunda mtazamo wao wa kisiasa, jambo linaloonyesha kuwa maamuzi ya kisiasa kwa kizazi hiki ni ya kijamii zaidi kuliko ya mtu binafsi.

Licha ya taarifa mpya, zana mpya na ari mpya, kikwazo kikuu bado kinabaki kuwa kuingia kwenye sajili ya wapiga kura.

“Wanaamini kuwa wana wajibu kama raia. Wanajua wanapaswa kushiriki katika mabadiliko, lakini bado wanasubiri wagombea wanaostahili kura yao,” anaongeza Bi Jerotich.

Utafiti ulijumuisha washiriki 531 kupitia mahojiano ya moja kwa moja, ukitoa taswira ya wakati halisi kuhusu hisia za kisiasa za vijana. Washiriki walikuwa na umri wa miaka 18–29 kutoka kaunti 20 zinazojiandaa kwa chaguzi ndogo za Novemba 27.

Hofu kuhusu usajili wa wapiga kura inatokea wakati wa shinikizo kubwa kisiasa. Takwimu za IEBC zinaonyesha kuwa asilimia 31 ya vijana waliotimiza umri wa kupiga kura hawataki kujisajili, jambo linaloleta wasiwasi mkubwa.

Bw Marjan Hussein Marjan, Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, anatoa wito kwa wazazi, taasisi na watu maarufu kuhamasisha vijana. Anasema bila utulivu wa kisiasa, hakuna uwekezaji unaoweza kustawi, jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa Ruwaza ya2030.

Upinzani nao unashutumu IEBC kwa kushindwa kutoa elimu ya uraia na kuanzisha ghafla teknolojia ya kunasa mboni za jicho bila maelezo ya kutosha, sambamba na muda mfupi wa usajili unaowazuia wanafunzi na wafanyakazi.

Hata hivyo, Bw Marjan anasisitiza kuwa tume ina mifumo thabiti ya kulinda data, kuongeza uwazi na kuzuia udanganyifu.

“Uchaguzi wa kuaminika huanza na data safi na sahihi. Teknolojia husaidia kuzuia usajili mara mbili, kukabiliana na hatari na kuboresha uwazi,” anasema.