Habari

IEBC yaanza kusambaza vifaa vya kura katika chaguzi ndogo

Na FRIDAH OKACHI November 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeanza kusambaza vifaa vya uchaguzi kutoka ghala lake kuu jijini Nairobi ili kufika katika vituo mbalimbali vya kupigia kura katika chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2025.

Maafisa wa IEBC wanasema vifaa vyote vitawasili katika maeneo ya uchaguzi kwa wakati ili kuruhusu maandalizi ya kutosha kabla ya siku ya kupiga kura.

Tume pia imewahakikishia wananchi uwazi na kuzingatia miongozo ya uchaguzi katika zoezi hilo lote.

Kamishna wa IEBC Bw Hassan Noor Hassan alisema walipokea jumla ya masaduku 39 ya karatasi za kupigia kura ya maeneo 22 ya uchaguzi kutoka kwa mshapishaji na kukaguliwa na kuthibitishwa kulingana na hati rasmi za usafirishaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua usafirishaji, Bw Noor alitangaza kuwa shehena la kwanza la karatasi za kupigia kura ilisafirishwa kuelekea eneo Bunge la Fafi katika Kaunti ya Garissa, mojawapo ya maeneo yanayoaminika kuwa mbali zaidi.

Aliwahakikishia Wakenya kuwa IEBC imejiandaa kikamilifu kwa chaguzi ndogo. Mafunzo ya maafisa wa uchaguzi yanaendelea, na maafisa wa usalama wamepewa maelekezo ya kutosha. Kila shehena la karatasi za kupigia kura itasindikizwa na maafisa wa usalama wa cheo cha juu kutoka ghala hadi eneo husika.

“Tangu zilipowasili, karatasi za kupigia kura zimekuwa zikilindwa saa 24. IEBC iko tayari kabisa. Tunataka kuwahakikishia Wakenya kuwa tuko tayari kwa chaguzi ndogo,” aliongeza afisa huyo.