Oburu atua Dubai kwa mapumziko mafupi familia ikikanusha anaugua
Kiongozi wa Chama cha ODM, Oburu Oginga, ameenda Dubai kwa mapumziko mafupi baada ya kile familia na wasaidizi wake wanataja kuwa “kalenda nzito na shughuli nyingi za kisiasa” katika wiki chache zilizopita.
Dkt Oginga, 82, ambaye amekuwa akihudhuria mfululizo wa mikutano mikubwa ya chama, ya kanda na ya kitaifa, alithibitisha mapumziko hayo Ijumaa na kusisitiza kwamba yuko katika hali nzuri ya kiafya.
“Najisikia mwenye shukrani kwa afya njema. Nachukua mapumziko mafupi ili kutafakari, kujipa nguvu na kujirekebisha upya,” Dkt Oginga aliandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.
Kumekuwa na tetesi kuhusu hali ya afya ya mwanasiasa huyo mkongwe.
Mwanawe ambaye pia ni msaidizi wake, Elijah Oburu, alikanusha taarifa zozote zinazoashiria kwamba anaugua.
“Ni kweli. Hajaugua. Siwezi kukupotosha,” Elijah aliambia Taifa Leo akisema kuwa Seneta huyo wa Siaya alichukua tu muda wa kupumzika baada ya wiki kadhaa za majukumu mazito.
Uamuzi wa Dkt Oginga kupumzika kwa muda mfupi unajiri baada ya kuzuru kaunti mbalimbali na kuongoza mikutano muhimu ya chama. Seneta huyo aliongoza maandalizi na shughuli za sherehe za siku nne za ODM@20 zilizofanyika Novemba 13–16 mjini Mombasa.
Maadhimisho hayo ya kuadhimisha miaka 20 tangu kuzaliwa kwa ODM yalikutanisha uongozi wa chama kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Wakati wa sherehe hizo, Seneta wa Siaya alishiriki vikao vya kuweka mikakati vilivyofanyika faraghani, mikutano na maafisa wa chama, na hafla za umma zilizofuatana.
Watu wa karibu chamani wanasema mwanasiasa huyo mkongwe hakupumuzika baada ya kutoka Mombasa kabla ya kurejea tena uwanjani kuendesha kampeni.
Siku chache tu baada ya maadhimisho hayo, Jumatano Novemba 19, Dkt Oginga alikuwa Kasipul ambako alijiunga na kampeni za ODM kumpigia debe mgombeaji wa chama hicho Boyd Were kuelekea uchaguzi mdogo, na akafanya misururu ya mikutano katika eneo bunge na viongozi wa mashinani.
“Ninaamini kwa dhati katika uongozi wa vijana—ndio mustakabali wa chama cha ODM. Ndiyo maana tulimuunga mkono Boyd Were katika uchaguzi mdogo wa Kasipul. Boyd, kama kijana mwingine yeyote katika chama chetu, anastahili kuungwa mkono, kutiwa moyo na kulelewa,” alisema.