Jamvi La Siasa

Chaguzi ndogo zinazotia vigogo tumbojoto

Na JUSTUS OCHIENG, BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Huenda chaguzi za Novemba 27 zikawa  ndogo, lakini hatari ya kisiasa inaweza kuwa kubwa zaidi kwa viongozi wakuu nchini.
Wakati kampeni rasmi zitakapofikia kikomo Jumatatu, Novemba 24, kabla ya uchaguzi mdogo wa Alhamisi, viongozi wakuu wa kisiasa, akiwemo Rais William Ruto, vinara wa Muungano wa upinzani chini ya aliyekuwa naibu Rigathi Gachagua, na chama cha ODM cha Oburu Odinga, watakuwa katika mtego mkubwa huku viti vikishindaniwa vikali.

Kile ambacho  kinaonekana kama uchaguzi wa kawaida wa maeneobunge na wadi  kimegeuka kuwa mtihani mkubwa kwa viongozi wenye nguvu zaidi kisiasa nchini, Rais Ruto, Gachagua, Naibu Rais Prof Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, na uongozi wa ODM baada ya Raila Odinga.

Kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wagombeaji 181 wameidhinishwa kugombea katika maeneo 24 ya uchaguzi, ikiwemo kiti cha Seneti cha Baringo, maeneo bunge sita  ya Mbeere Kaskazini, Malava, Kasipul, Ugunja, Magarini na Banisa na wadi 17.
“Kampeni zitamalizika Jumatatu, Novemba 24, 2025, ikiwa ni saa 48 kabla ya siku ya uchaguzi mdogo,” alisema Meneja wa Operesheni za Uchaguzi wa IEBC Gideon Balang.

Lakini chini ya makaratasi ya IEBC kuna vita vikali vya kisiasa vya kulinda ushawishi na kudhibiti hali.

Viti vinavyoshindaniwa zaidi ni Mbeere Kaskazini na Malava ambavyo vimegeuka kuwa mapambano ya moja kwa moja kati ya Rais Ruto na Gachagua.

Katika Mbeere Kaskazini, Dkt Ruto amemteua naibu wake, Prof Kindiki, kushughulikia ushindi wa mgombeaji wa serikali, na hivyo kufanya uchaguzi huo kuwa kipimo cha uzito wa kisiasa wa msomi huyo aliyegeuka mwanasiasa katika Mlima Kenya Mashariki na, kwa upana, uwezo wake kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto katika uchaguzi wa 2027.

Kushindwa kwa mgombeaji wa serikali Mbeere Kaskazini pia kunaweza kuwa tisho kwa Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire ambaye ni gavana wa kaunti ya Embu.

Msaidizi wa karibu wa Rais Ruto, Farouk Kibet, amepiga kambi Malava kwa wiki kadhaa akisimamia kampeni za UDA kana kwamba eneo bunge hilo ni uchaguzi wa kitaifa.

Kwa upande mwingine, Gachagua, anawaunga mkono wagombeaji wa muungano wa upinzani.
Malava, ambapo washirika wake wa upinzani wamewasilisha mgombeaji mwenye nguvu, ni kipimo muhimu cha iwapo Gachagua, aliye kuwa naibu rais, anaweza kupenya ngome za jadi za Ruto.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa kushindwa kwa upande wa Dkt Ruto katika Mbeere Kaskazini au Malava kutakuwa pigo kwa serikali  na ushindi kwa Gachagua.
Kinyume chake, kushindwa kwa upinzani kutadhoofisha uhalali wake kama nguvu ya kisiasa ya kweli.

Dismas Mokua, mchambuzi wa kisiasa anasema “kila kambi ina jukumu kubwa la kushinda viti hivi muhimu.”

Mudavadi pia ana presha. Malava iko katika eneo lake la Magharibi ya Kenya, na siku zake za kisiasa zitategemea iwapo ataweza kuvuma katika ukanda huo licha ya umaarufu unaoongezeka wa upinzani.
DAP-K imemwasilisha Seth Panyako, katibu mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi Kenya, ambaye kampeni yake imepata umaarufu.
UDA inamuunga mkono David Ndakwa. Kushindwa kwa Mudavadi kulinda kiti hiki kwa UDA kutazua maswali kuhusu umuhimu wake ndani ya Kenya Kwanza.

Chaguzi hizi ndogo pia zitakuwa mtihani wa kwanza mkubwa wa ODM kufuatia kifo cha kiongozi wake Raila Odinga mnamo Oktoba 15 nchini IndiaODM imekuwa ikitegemea sana ushawishi binafsi wa Odinga. Viongozi wa chama sasa wanahimiza wafuasi kuheshimu “baraka za mwisho za Baba,” kwa kuchagua wagombeaji wa ODM -Boyd Were (Kasipul), Moses Omondi (Ugunja), na Harrison Kombe (Magarini) alioidhinisha muda mfupi kabla ya kifo chake.

“Kushindwa kwa ODM katika viti hivi kutazua wasiwasi kuhusu mustakabali wa chama katika baada ya Raila,” anasema Mokua.
Mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga amewaambia wapiga kura “kuchagua wagombea wa ODM kuheshimu urithi wa Raila Amollo Odinga.”