Habari za Kitaifa

Matiang’i akemea vurugu za uchaguzi , aonya serikali

Na RUTH MBULA November 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee na mgombeaji wa urais Dkt Fred Matiang’i amemwambia Rais William Ruto akomeshe  washirika wake wanaozua ghasia za kisiasa, la sivyo watasababisha janga.

Akizungumza katika Kanisa la SDA la Tonga Kaunti ya Nyamira, Jumamosi, Dkt Matiang’i alielezea huzuni kwamba serikali inavumilia ghasia za kisiasa kwa manufaa ya muda mfupi.

“Nashauri serikali: ikiwa hamtaacha vitendo hivi, mtaleta janga. Mmeanzisha shida ambayo hamwezi kuepuka. Sasa mnafikiria kwa sababu mko madarakani, mnaweza kutishia na kununua watu,” alionya Dkt Matiang’i.

Waziri huyo wa zamani alilalamikia kwamba watu walishambuliwa katika Magharibi mwa Kenya na wahuni waliokuwa na silaha mbele ya maafisa wa usalama.

“Ni aibu kwamba serikali inajihusisha na vurugu yenyewe, ikipanga wahuni na kuhonga wananchi. Huu ndio mwanzo wa mwisho. Mwanzo wa kushuka kwenu uko hapa. Serikali haiwezi kudhulumu watu ambao inapaswa kuongoza,” alisisitiza.

Aliongeza, “Asubuhi ya leo, wakati Gavana wa Trans Nzoia, Natembeya alikuwa akifanya kampeni huko Kabuchai, nilifanya kazi katika sekta ya usalama, na hamuwezi kuniambia kwamba kamishna wa kaunti na timu ya usalama hawakuwa na habari ya kilichotokea huko. Kisha wanajifanya kwamba kulikuwa na fujo kati ya makundi mawili.”

Dkt Matiang’i alisema walishambuliwa walipokuwa Malava Ijumaa, lakini wananchi walikataa ghasia zilizoendeshwa na serikali.

Waziri huyo wa zamani aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufuatilia shughuli haramu  zinazoendelea katika kampeni za uchaguzi mdogo katika Kaunti ya Nyamira.

Dkt Matiang’i alidai kuwa baadhi ya wafuasi wa Kenya Kwanza walikuwa wakitumia mamilioni ya pesa katika kampeni zao, huku Kiranja wa Wengi na Mbunge wa South Mugirango, Silvanus Osoro, akiahidi wazi kutumia njia zisizo za kiungwana kuhakikisha wagombeaji wao watatangazwa washindi, hata kama watashindwa kwenye sanduku la kura.

Kuna uchaguzi mdogo utakaofanyika  27 Novemba 27 katika wadi za Nyamaiya, Ekerenyo, na Nyansiongo.

Majuzi, Bw  Osoro alisema katika mikutano ya kampeni kkwamba chama chake kina “njia nyingine” za kutangaza wagombea wao washindi, hata kama watashindwa kwenye kura.

Dai hili limeleta taharuki kwa timu ya Matiang’i, ambayo imeeleza hofu kwamba serikali inajaribu kutumia mamlaka yake kudanganya katika uchaguzi na hatimaye kumuonyesha Dkt Matiang’i kama dhaifu  nyumbani kwake.