Jamvi La Siasa

Gachagua, Kindiki sasa wafufua vita vya ubabe mlimani

Na  GEORGE MUNENE, BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VITA vya ubabe kati ya Naibu Rais Kithure Kindiki na mtangulizi wake Rigathi Gachagua vimeibuka upya, huku Kindiki akitangaza kwamba ndiye msemaji wa eneo la Mlima Kenya.

Uwanja wa mapambano ni Mbeere Kaskazini ambapo wakazi wanajiandaa kumchagua mbunge wao.Akizungumza katika soko la Kanyuambora alipokuwa akipigia debe mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Leonard Muthende, Naibu Rais Kindiki alimshambulia Gachagua, akimshutumu kwa kujitangaza Msemaji wa wakazi wa eneo hilo.

“Gachagua anapaswa kuacha kudanganya watu, mimi ndiye Mfalme wa Mlima,” alisema.Kindiki alisisitiza kwamba amekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu kuliko Gachagua, na kwa hivyo yeye ndiye anayeweza kuzungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

Profesa Kindiki alimkumbusha Gachagua kwamba yeye ndiye kiongozi mkuu zaidi katika ukanda huo akiwa na uzoefu mkubwa wa uongozi na siasa.

“Nimekuwa seneta, Naibu Spika, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Waziri na sasa Naibu Rais, huku Gachagua akiwa mbunge wa muhula mmoja tu ambaye hapaswi kuongoza Mlima,” alisema.

Profesa Kindiki alidai kwamba Gachagua alipoteza heshima yake alipomdharau Rais Ruto, na anapaswa kuacha kulalamika.Lakini Gachagua alisisitiza kwamba bado ndiye Kiongozi halali wa Mlima na ameahidi kuendelea kuongoza wakazi kisiasa.

“Mimi ndiye msemaji wa Mlima na niko hapa kuwaambia wananchi wa Mbeere Kaskazini ukweli, Newton Kariuki wa DP ni mgombeaji wa muungano wa upinzani na ndiye mtu sahihi kutwaa kiti cha Mbunge,” alisema Gachagua katika soko la Kamumu.

Aliahidi kumfundisha Kindiki somo wakati wa uchaguzi mdogo.Gachagua aliwaambia Kindiki na wafuasi wake wajiandae kwa uchaguzi mgumu Novemba 27.

“Nitathibitisha kwa Kindiki kwamba ni mimi ninayedhibiti Mlima wakati mgombeaji wa UDA atashindwa uchaguzi wa kiti cha Ubunge,” alisema Gachagua. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku alikosoa upinzani akiwashutumu kwa kudanganya wakazi wa Mbeere Kaskazini na kujaribu kuwatenga na serikali inayowapa maendeleo kwa vitendo.

Alisema wananchi wa Mbeere Kaskazini wana busara na hawawezi kushawishiwa na maneno ya uongo, na wataendelea kuunga mkono serikali katika kuhakikisha miradi ya sasa na ya baadaye inatekelezwa.

Ruku alikosoa pia madai ya upinzani kwamba serikali haifanyi kazi, akisema ni mbinu za kudanganya kuwachanganya wapiga kura.Alisisitiza kwamba kampeni za UDA zinalenga amani na maendeleo, akibainisha kwamba wakazi wa Mbeere Kaskazini siku zote wamekuwa wa amani.