Jamvi La Siasa

Oburu aenda likizo mawimbi yakipiga

Na BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kuongoza shughuli nzito ya mazishi ya kaka yake Raila Odinga na misururu ya hafla za kisiasa kama kiongozi mpya wa chama cha ODM, Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga ametangaza kuanza likizo kutafakari.

“Ninajihisi mwenye shukrani kwa sababu ya afya njema na moyo wa furaha. Naanza mapumziko mafupi ili kutafakari, kujipatia upya nguvu na kuanza upya,” Dkt Oburu alitangaza kupitia mtandao wa X.

Haya yanajiri wakati ambapo amejipata katika mawimbi makali akiwa kinara wa ODM na pia familia ya Jaramogi Oginga Odinga.ODM inakumbwa na mawimbi makali yanayotishia kuisambaratisha, madai ya usaliti, njama za kuuza chama, na mvutano kuhusu mustakabali wa ushirikiano wake na serikali ya Kenya Kwanza.

Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya chama mjini Mombasa, Oburu alisema hajapata nafasi ya kuomboleza kifo cha ndugu yake kutokana na shinikizo la kisiasa ndani ya ODM.

“Kufika hapa mbele yenu, kwanza nimefika kama mwanzilishi wa ODM. Hadi sasa sijaamini Raila hayuko. Mimi bado nalia,” alisema kwa huzuni.Oburu alisisitiza kuwa alikuwa katika kila hatua ya safari na Raila—kampeni, mapambano na misukosuko—na yuko tayari kuongoza ODM baada ya kifo chake.Ndani ya chama, amekosolewa na baadhi ya viongozi wanaoonekana kujitokeza kutwaa usukani.

Akiwa na hisia kali, Winnie Odinga, binti ya mwisho wa Raila, alilipua bomu la madai mazito kwamba kuna vigogo ndani ya chama wanaopanga kuuza ODM kwa siri.Akiongea mbele ya umati mkubwa Mombasa, Winnie alisema chama hiki hakikuzaliwa kwenye vyumba vya siri, wala hakikuwa mradi wa watu wachache.

“Nimejulishwa kwamba wako wanaotembea nasi mchana, lakini usiku wanapanga kuuza ODM. Hilo halitawezekana,” alisema huku akipigiwa makofi.Kwa mujibu wake, mustakabali wa ODM unazungumzwa kwenye mikutano ya usiku na mazungumzo ya siri jambo linalodaiwa kuhusisha wale wanaounga mkono ushirikiano wa sasa na serikali ya Rais Ruto.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna naye hakuficha hasira zake kuhusu misimamo inayokinzana ndani ya chama, akisema hakiko tayari kugeuzwa tawi la Kenya Kwanza wala kiungo kinachotegemea maamuzi ya watu wachache.Akiashiria wazi kwamba chama kinaweza kusimama pekee yake bila kuwa chini ya kivuli cha serikali, Sifuna alisema

“Sitafuata serikali kipofu. ODM ina uwezo wa kusimamisha mgombeaji wa urais mwaka 2027.”Kwa upande wake, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, mmoja wa wakosoaji wakuu wa ushirikiano wa ODM na serikali, alitoa matamshi yanayotishia mpasuko zaidi.Amisi alidai kuwa Raila Odinga “aliacha chama mikononi mwa watu wasiostahili” na kusema uongozi wa sasa “hautamruhusu Raila apumzike kwa amani.”

Aliongeza kuwa ifikapo mwaka 2026, kutakuwa na “hali ya dharura” ya kisiasa ndani ya chama, akisisitiza kuwa chama lazima kijiondoe kwenye makubaliano ya Serikali Jumuishi.

Kwa sasa, ODM kinaonekana kugawanyika katika makundi mawili makuu:Kundi la wanaotaka kushirikiana na serikali ya Ruto, Kundi la wakereketwa wa upinzani wa kiasili linachoongozwa na Sifuna, Winnie na Gavana wa Siaya James Orengo.

Kwa wachambuzi wengi wa siasa, likizo ya Oburu imeonekana kama hatua ya kupisha baridi hali itulie hasa baada ya ishara kuwa misukosuko imefika ndani ya familia ya Jaramogi yenyewe ambayo ilionekana kuungana chini ya marehemu Odinga.

“Huku Winnie akitaka mikutano ya siri usiku kuhusu ODM ikomeshwe na kikao cha wajumbe wa kitaifa kiandaliwe kuchagua viongozi, Sifuna anasisitiza ODM isiungane na Ruto 2027, na Amisi akionya kuwa chama kinaelekezwa shimoni, mawimbi ndani ya chama yanaonekana kuongezeka,” asema mchanganuzi wa siasa Betty Odhiambo.