Jamvi La Siasa

Haki ningesikiliza Ruto akisema uongo bungeni ningechemka, asema Sifuna

Na BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SENETA wa Nairobi na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, amesema alikataa kusikiliza hotuba ya Hali ya Taifa ya Rais William Ruto akiitaja kama “uongo mtupu” uliogeuza hafla hiyo kuwa uzinduzi wa manifesto ya kampeni ya urais ya 2027.

Kulingana na Sifuna, endapo angesikiliza hotuba hiyo angeghadhabika “na kupigwa marufuku kuhudhuria vikao vya seneti kwa miezi sita” kwa kuyapinga hadharani madai ya Rais.

“Mimi nilikataa kusikiza uongo ya Ruto kwa sababu ningechemka nitolewe kwa miezi sita. Unawezaje kuzungumzia elimu kubadilisha Kenya iwe kama Singapore na hata masuala yanayoathiri shule na vyuo huawezi kushughulikia? Vyuo Vikuu vya Kibinafsi vina madeni ya Sh60 bilioni halafu unakuja kutuambia maneno ya Singapore, huyo ni mtu anaelewa kitu anafanya kweli?” alihoji Sifuna.

Alidai kwamba hotuba ya Rais haikuwa tathmini ya utendaji bali ilikuwa ni madai yaliyopangwa “kupotosha umma” kuhusu hali halisi ya uchumi, elimu, afya na miundomsingi.

Mbunge wa Saboti Caleb Amisi alidai kuwa Rais alitumia hotuba ya kitaifa “kuzindua manifesto ya kutafuta kura,” akisema hilo halijawahi kutokea.“Rais anatumia hotuba ya Hali ya Taifa kuzindua manifesto ya kuchaguliwa kwake tena, haijawahi kufanyika, halafu wabunge wanampigia makofi, hao walikuwa wamelipwa,” alisema Amisi.

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba naye alisema alishtuka Rais alipodai kuwa mauzo ya majani chai nchini yaliongezeka kwa asilimia 54.Kwa upande wake,

Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Antony Kibagendi alisema Rais “aliwadanganya Wakenya,” akidai alitoa takwimu za kupotosha kuhusu ajira za Wakenya 400,000 barani Asia na kushindwa kurekebisha mfumo wa ufadhili wa elimu ya juu.

Viongozi hao, waliokuwa wakihudhuria hafla ya kuwasaidia wajane katika uwanja wa shule ya upili ya Magina, Kisii walisema pia kwamba nafasi ya ODM ndani ya serikali jumuishi inatathminiwa upya—na hakuna uhakika kuwa chama hicho kitaendelea kuwa ndani ya mpango huo mwaka ujao.