Jamvi La Siasa

Washindana kufasiri matakwa ya mwisho ya Raila

Na  MOSES NYAMORI November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Kutafsiri matakwa ya mwisho na maono ya kisiasa ya aliyekuwa kinara wa upinzani, Raila Odinga, kumekuwa silaha muhimu ya kisiasa inayoweza kuathiri uchaguzi wa urais wa 2027 na mpangilio wa urithi ndani ya chama cha ODM.

Kwa mwezi mmoja tangu kifo chake mnamo Oktoba 15, wanasiasa wakuu, akiwemo Rais William Ruto, wameendelea kutaja jina lake wakijaribu kushawishi mjadala wa nani atarithi wafuasi wake wengi.

Tayari, makundi mawili yamejitokeza:Kundi la kwanza linataka kudumisha misingi ya upinzani aliyosimamia Raila ya mapambano ya haki za kijamii, demokrasia na utawala bora huku kundi la pili likitaka ODM ikubaliane na “hali halisi mpya” kupitia serikali jumuishi , hali ambayo huenda ikafanya chama kuendelea kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.

Wachambuzi wanabainisha kuwa urithi wa Raila unatafsiriwa kwa njia tofauti na makundi ndani ya ODM, serikalini na upinzani, kila moja likitafuta maslahi yake kuelekea uchaguzi wa 2027.Mwelekeo huu, wanasema, utachangia kuamua kama ODM itamuunga mkono Rais Ruto kutetea kiti au ijiondoe serikalini na kusimamisha mgombeaji wake.
Hii pia ina uwezo wa kuathiri namna wafuasi wa jadi wa Raila watakavyopiga kura mwaka huo.

Katika hotuba yake Hali ya Taifa Alhamisi, Rais Ruto alimrejelea Raila, akieleza jinsi mazungumzo yao yalivyochangia mpango wake wa Sh5 trilioni wa kufanya Kenya kuwa taifa lililoendelea.

“Nilijadili maono haya na marehemu Raila Odinga, ambaye alinikumbusha kuwa hakuna taifa linaweza kuendelea bila barabara, umeme na utoshelevu wa chakula,” alisema, akiongeza kuwa pia alishauriana na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu umuhimu wa kuimarisha uwekezaji wa miundombinu.

Lakini afisa mmoja wa ngazi ya juu wa ODM, aliyezungumza kwa sharti ya kutotajwa jina kutokana na uzito wa suala hilo, aliambia Taifa Leo kuwa hakuna uhakika iwapo Raila angeunga mkono Ruto mwaka 2027.

Afisa huyo anasema maslahi ya Raila yalikuwa kwenye Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu utekelezaji wa ajenda ya vipengee 10 na Serikali Jumuishi hadi 2027.“Raila alikuwa wazi kuhusu aina ya ushirikiano aliokuwa nao na UDA. Alikataa kuingia mkataba wa ushirikiano wa kisiasa na kusisitiza MoU ya kutatua masuala ya wananchi—kama fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi,” alisema.

Katika hotuba yake ya mwisho hadharani mnamo Septemba 22, 2025, Raila aliwakumbusha wanachama wa ODM kusoma na kufuata hoja za MoU ya Machi 2025 ambayo, alisisitiza, haikuhusu uchaguzi wa 2027.“Hatuna uamuzi kama chama kuhusu jinsi tutakavyoingia uchaguzi wa 2027. Msikubali kuingiza chama kwenye makubaliano ambayo hayajajadiliwa,” alisema.

“Nani aliwaambia ODM haitakuwa na mgombeaji mwaka 2027? Tuna mpango tuliojadiliana; maamuzi mengine yatakuja wakati ufaao.”Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa serikali Jumuishi, amependekeza chama kiongozwe na yale Raila aliyosema hadharani badala ya maelezo ya faraghani.

“Watu wengi wanaeleza alichowaambia binafsi. Kwa kuwa hatuwezi kukubaliana kila mmoja na simulizi lake, tufuate alichotuambia hadharani, kutunza ODM kama taasisi huru,” alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM.

Naibu kiongozi mwenza wa ODM Godfrey Osotsi aliambia Taifa Leo kuwa Raila aliwasiliana na watu wengi, lakini ujumbe wake ulikuwa thabiti: kutaka serikali itekeleze vipengee 10 vya MoU. Bw Osotsi alisema kuwa “Baba (Raila) aliwaeleza watu wengi mambo tofauti, lakini ujumbe wake ulikuwa thabiti kila mara. Watu wasipotoshe alichosema kwa vile sasa hayupo.”

Aliongeza kuwa Raila alisisitiza ODM ijijenge upya kuelekea uchaguzi wa 2027, ndiyo maana alikuwa ameelekeza nguvu kwenye chaguzi za ndani ya chama. Kwa mujibu wake, Serikali Jumuishi si muungano wa kisiasa, na chama kitaamua wakati ufaao kuhusu namna kitakavyoingia katika uchaguzi wa 2027.

Katika mazishi ya Bw Odinga, viongozi kadhaa wa ODM akiwemo Mwenyekiti wa Kitaifa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Kiongozi wa Wachache Bungeni Junet Mohammed, na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir waliwaambia waombolezaji kuwa matakwa ya mwisho ya Raila yalikuwa waendelee kufanya kazi na Rais Ruto.


“Tumekuwa tukimfuata Raila kila mara. Maagizo yake ya mwisho ni tushirikiane na wewe (Ruto) ndani ya serikali jumuishi,” alisema Bi Wanga.
 Aliongeza kuwa wanachama wa ODM wanashikilia wizara muhimu serikalini kama vile Wizara ya Fedha, inayosimamiwa na Waziri John Mbadi, na usalama kupitia Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo, na kusisitiza kuwa “hapo ndipo Raila alituambia tuwe.”

Mnamo Ijumaa, Bw Mbadi alisema ana sifa zote za kuwa ‘mfalme wa siasa’ eneo hilo. Alisema:
 “Ninajua Raila alikuwa anatuelekeza wapi, najua njia alizokuwa anafuata. Sitavaa viatu vyake; nitanunua vinavyonifaa na kuongoza jamii ya Waluo kwa njia ninayojua, tunapoingia Canaani.”

Profesa David Monda, mhadhiri na mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika, alisema hata enzi za uhai wake Raila aliwaacha wengi wakikisia hatua yake ya kisiasa ya mwisho.


 “Mbinu yake ya kutokuwa wazi kuhusu malengo yake ya mwisho ya kisiasa hadi dakika za mwisho sasa imegeuka kuwa udhaifu mkubwa wa ODM. Kwa kuwa Raila alikuwa akitumia mkakati wa ukimya wa kisiasa, kifo chake cha ghafla kimeacha kila mtu akijiuliza ni nini alitaka kifanyike katika ODM,” alisema.

Aliongeza kuwa hatari hii inatokana na ukweli kwamba ODM haikujengwa kimsingi kwa misingi ya kiitikadi, bali kwa nguvu za kiongozi mmoja ambaye sasa hayupo.

Prof Monda alibainisha kuwa washirika kadhaa wa karibu wa Raila, wakiwemo walioteuliwa serikalini kama John Mbadi (Hazina), Opiyo Wandayi ( Kawi) na Hassan Joho (Madini), wanaonekana kutaka kuendelea kusimama upande wa Rais Ruto.