Habari za Kitaifa

Ruto alipanga njama ya Ruto kunivua wadhifa wangu ODM, adai Sifuna

Na RUTH MBULA November 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, sasa anadai kwamba Rais William Ruto alipanga njama ya kumuondoa katika wadhifa wake kama Katibu Mkuu wa Chama cha ODM.

Akizungumza Ijumaa wakati wa harambee ya kuwasaidia wajane katika eneobunge la Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii, Bw Sifuna alidai kuwa wandani wa Rais walipanga kutekeleza njama hiyo wakati wa hafla ya chajio ya waanzilishi wa ODM iliyofanyika hivi majuzi Mombasa.

“Tulifanya mkutano huo Jumapili au Jumamosi usiku — je, Sifuna bado ni Katibu Mkuu ama sivyo?” aliuliza.

Katibu Mkuu huyo wa ODM, aliyekuwa ameandamana na wanachama wa vuguvugu la Kenya Moja Alliance, alidumisha msimamo mkali dhidi ya kile alichokitaja kama utawala mbovu wa Rais Ruto.

Wabunge Caleb Hamisi (Saboti), Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu), Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini) na Gathoni wa Muchomba (Githunguri) walihudhuria hafla hiyo.

Matamshi hayo makali ya Bw Sifuna na wenzake yanajiri licha ya chama cha ODM kuwa katika ushirikiano na chama tawala cha UDAchini ya Serikali Jumuishi.

Rais Ruto alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa ODM waliohudhuria katika hafla ya chajio iliyofanyika Mombasa Jumamosi iliyopita.

ODM ilikuwa ikiadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kupitia sherehe za siku tatu katika bustani yaMama Ngina Waterfront, kuanzia Ijumaa hadi Jumapili, ikiwa ni kumbukumbu ya kile ilichokitaja kama miongo miwili ya huduma na mapambano ya kisiasa. Maadhimisho hayo yalijikita katika urithi wa marehemu kiongozi wa ODM, Raila Amolo Odinga.

Bw Sifuna alisema yuko tayari kushirikiana na kiongozi yeyote atakayesaidia kumuondoa Rais Ruto mamlakani, akiwemo *Dkt Fred Matiang’i.

“Nilikuwa KICC wakati ODM ilitia saini makubaliano na chama cha UDA. Katika ajenda hiyo ya vipengele 10, Rais William Ruto hakutaja hata kipengele kimoja wakati wa hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa bungeni Alhamisi,” alisema Bw Sifuna.

Seneta huyo wa Nairobi alidai kuwa utekaji nyara na mauaji ya vijana bado yanaendelea nchini kinyume na makubaliano hayo.

“Mimi ndiye niliyeandika makubaliano yale na ninaendelea kufuatilia utekelezaji wake na kuweka alama,” alisema.

Aliwaonya viongozi wa ODM ambao bado wanaunga mkono serikali jumuishi, akisema hakuna mtu anayejua kwa kina makubaliano kati ya Rais Ruto na Raila Odinga.

“Ni William Ruto na Raila Odinga pekee ndio wanajua walikubaliana nini. Wengine walikuwa watazamaji tu. Sasa ninyi watazamaji, hatuwaogopi; mkiongea mnatisha kuwa mtaondoa Sifuna na mimi chamani kwa sababu tunawaambia ukweli,” akasema Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi.

Akaongeza: “Ni Baba pekee aliyejua Serikali Jumuishi ikiugua i na lini kuipeleka hospitalini. Ni yeye tu aliyekuwa akijua lini serikali jumuishi inapaswa kupewa dawa ya malaria. Msiseme ODM kwamba tuko katika serikali jumuishi hadi 2027.”

Bw Hamisi alisema kuwa marehemu Bw Odinga alifanya kazi na serikali mbalimbali lakini kila mara alijiondoa.

“Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Baba kuingia serikalini. Alifanya kazi na Rais Daniel arap Moi na akaondoka mwaka mmoja kabla ya uchaguzi. Alifanya kazi katika serikali ya muungano na Rais Mwai Kibaki lakini akaondoka. Alifanya kazi pia na Rais Uhuru Kenyatta,” akasema, akidai kuwa marehemu kiongozi huyo wa ODM angeondoka kwenye Serikali Jumuishi kufikia Machi 2026.