Makala

Jinsi ya kufunza mtoto busara mtandaoni

Na BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Watoto na matineja wamezungukwa na teknolojia kila mahali, na ni muhimu kuwasaidia wajenge ujuzi wa kuitumia kwa usalama.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO, 2018), ufahamu wa kidijitali ni uwezo wa kupata taarifa, kuitumia, kuielewa, kuwasiliana na kuiunda kwa njia salama kupitia teknolojia.

Kama ilivyo katika maadili mengine ya maisha, wazazi wana jukumu la kuwafunza watoto namna ya kutumia mtandao kwa busara kupitia mazungumzo ya mara kwa mara, yanayoendana na umri.

Mazungumzo haya huwapa watoto nafasi ya kuelezea wanachokiona mtandaoni na kuwaonyesha kuwa uzoefu wao wa kidijitali unathaminiwa.

Lakini wazazi wanapaswa kuzungumza nini wanapowajengea watoto uelewa wa usalama mtandaoni? Haya ndiyo mambo muhimu

1.Linda taarifa binafsi

Watoto wafahamu kuwa anuani, nambari za simu, taarifa za shule au pesa si vitu vya kusambazwa mtandaoni. Watoe habari hizi tu kwa watu wanaowafahamu vyema.

2.Sio kila mtu mtandaoni alivyo anavyojitambulisha

Kuna watu wenye nia mbaya. Mtu anayeonekana kama kijana wa rika lako anaweza kuwa mtu mzima mwenye madhara. Vijana waelemishwe kuhusu hatari ya kuzungumza na watu wasiowajua.

3.Kila kitu kikitumwa mtandaoni kinaweza kusambaa

Picha, ujumbe na video vinaweza kunaswa kwa “screenshot.” Wazazi wafunze watoto kufikiri kabla ya kutuma kitu chochote.

4.Mtandaoni kuna maudhui yasiyofaa

Kuna mambo ya ngono, vurugu, dawa za kulevya, chuki na hata ushawishi wa kujidhuru. Watoto wajue kuwa wakikutana na maudhui mabaya wafichue kwa mtu mzima wanayemwamini.

5.Mitandao inaweza kulewesha

Teknolojia huamsha sehemu ya ubongo inayohusiana na starehe. Vijana waelezwe umuhimu wa kuweka mipaka, kupumzika na kutambua dalili za uraibu wa vifaa bebe.

6.Si kila habari mtandaoni ni ya kweli

Kuna taarifa potofu, picha bandia za AI na vichwa vya habari vya kupotosha. Watoto wafunzwe kuthibitisha habari kwa vyanzo zaidi ya kimoja.

7.Ukatili mtandaoni upo

Matineja wafahamu maana ya unyanyasaji mtandaoni na wajue hatua ya kwanza ni kumwambia mtu mzima anayeaminika.

Mazungumzo haya yanaweza kuanza kutokana na habari, masomo shuleni au kile mzazi ameona mtandaoni. Cha muhimu ni kuyafanya mazungumzo kuhusu matumizi ya mtandao kuwa sehemu ya maisha ya nyumbani.

Mwisho, wazazi na walezi wawe wazi kuhusu tabia zinazokubalika mtandaoni. Waongoze kwa mfano,watoto hujifunza zaidi kwa kile wanachoona wazazi wao wakifanya.