Pambo

Tumia simu kuboresha mapenzi, si kubomoa

Na BENSON MATHEKA November 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika enzi hizi ambapo mawasiliano hutegemea simu za mkononi, wataalamu wanasisitiza kwamba unavyotumia kifaa hiki kwa mwenzi wako inaweza kujenga uhusiano wenye afya au kuusambaratisha kabisa.

Huku simu zikiwa sehemu ya maisha ya kila siku, wataalamu wa mahusiano wanatoa tahadhari: simu inaweza kuwa daraja la mapenzi—au ukuta unaowatenganisha.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa mahusiano, Mwanasaikolojia  Jane Muthoni, tatizo si simu yenyewe bali tabia za watumiaji. “Watu wengi husema ‘nakukosa’ lakini hawafanyi lolote kuhakikisha mawasiliano yanaimarika,” asema.

“Kama unamkosa mwenzi wako, mpigie. Ujumbe mfupi mara nyingi hauna hisia sawa na sauti.”

Bi Muthoni anaongeza kuwa hata simu ya dakika moja inaweza kubadili siku ya mwenzi wako. “Wengi hudhani mazungumzo marefu ndiyo muhimu, lakini ukweli ni kwamba kusalimia tu kwa upole kunaleta hisia za kuthaminiwa.”

Mtaalamu wa tabia za kijamii, Patrick Mwangangi, anaonya dhidi ya kutumia simu kama zana ya kutiliana shaka. “Maswali kama ‘Ulikuwa wapi? Mbona hukuchukua?’ huanzisha mazungumzo ya uhasama,” anasema. “Mwenzi wako huvaa ukakamavu akijitetea, kana kwamba yuko kizimbani.”

Dkt Mwangangi pia anapinga tabia ya kumlazimisha mwenzi kutoa simu anapoongea na mtu mwingine kuthibitisha alichosema. “Hiyo ni dharau. Inaharibu kuheshimiana na kuonyesha kutoaminiana kwa kiwango cha juu.”

Kwa upande mwingine, kurejesha simu za mwenzi wako ni ishara ya heshima. Kumpigia au kutuma ujumbe baada ya kukosa simu yake ni hatua ndogo, lakini inaonyesha kwamba unamjali na humpa amani ya moyo.

Mtaalamu wa saikolojia ya familia, Daniel Obiero, anasema wengi wanaharibu mawasiliano kwa kutumia simu kwa ukatili.

“Simu zako kwa mwenzi hazipaswi kuwa za kutoa maagizo, lawama au maombi ya pesa pekee,” asema. “Anza kwa salamu changamfu. Ulizia hali yake. Haya mambo madogo hubeba uzito mkubwa.”

Obiero pia anaonya dhidi ya kukata simu wakati wa mabishano. “Hiyo ni ishara ya dharau,” asema. “Badala yake, sema kwa upole kwamba mazungumzo yanahitaji kupumzishwa ili yasiharibike zaidi. Ukarimu wa mwisho wa mazungumzo huamua kama mzozo utamalizika kwa amani au kwa sumu.”

Wataalamu wanaeleza kuwa simu za video za mara kwa mara huimarisha ukaribu, hasa kwa wanaoishi mbali. Kuona tabasamu la mwenzi wako husaidia kuvunja ukuta wa umbali na kuleta hisia za uwepo.

Tabia hii ya teknolojia hujenga mtazamo wa jinsi unavyomheshimu mwenzi wako. Mwanasaikolojia Muthoni anatoa wito watu wasionyeshe hasira wakati wa simu hizi au kuzifanya wakiwa mbele ya watu.

“Pigia mtu wako simu nyakati unazojua yuko peke yake kwa kuwa hatakuwa na cha kumsumbua. Usiwe na hasira unapopigia mpenzi wako simu ya video au simu yoyote ile,” asema.

Badala yake, mazungumzo ya simu yawe na utani, sauti ya upole na shukrani. “Mpenzi wako asisikie ukicheka sana na rafiki yako kwenye simu lakini ukiongea naye hauchangamki. Hicho ni chanzo cha maumivu ya moyo bila kujua.”

Katika dunia ya sasa, asema Prof Obiero, simu imekuwa sehemu ya uhai wa uhusiano.
Wataalamu wanakubaliana kwamba mawasiliano bora si wingi wa simu unazopigia mtu wako, bali ubora na uendelevu wake.

Wanasisitiza kwamba kizazi cha sasa kina bahati ya kuwa na teknolojia ambayo mababu zetu hawakuipata. “Tuitumie kuboresha mapenzi, si kuharibu,” asema Mwangangi.