Wandia, Rono waongeza dhahabu Deaflympics nchini Tokyo
LUCAS Wandia Wanjiru na Elikana Kiprop Rono waliwapa Wakenya raha baada ya kuongeza dhahabu za Kenya kufika nne kwa kunyakua dhahabu katika vitengo vyao kwenye Olimpiki za Viziwi (Deaflympics) jijini Tojkyo nchini Japan, Jumapili, Novemba 23, 2025.
Wandia alihifadhi taji la mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji naye Rono akaibuka namba wani katika 800m.
Wandia, 36, ambaye anashikilia rekodi ya Deaflympics ya dakika 9:04.82, alikata utepe kwa 9:06.95. Alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Jacob Kibet Kipkemoi (9:09.16) na Mchina Kuant Xu (9:09.88). Mkenya Joseph Gitau Ndungu alifunga nne-bora (10:18.32) kutoka orodha ya washiriki wanane.
Medali hiyo ni ya nne ya Wandia katika umbali huo baada ya kuvuna fedha mwaka 2013 jijini Sofia (Bulgaria) na dhahabu mwaka 2017 (Samsun, Uturuki), 2022 (Caxias do Sul, Brazil) na sasa Tokyo.
“Nimekuwa nikiomba Mungu sana nipate mafanikio haya. Si kazi rahisi. Kabla ya kuondoka Kenya, niliahidi nitaleta medali aina yoyote. Nafurahia kuwa nitarejea nyumbaji na dhahabu,” akasema Wandia.
Katika urushaji wa mkuki, Stephen Okoth alikamata nafasi ya 10 akiwa na mtupo wa mita 48.12 naye Hillary Chirchir akamaliza mkiani kwa 43.94m.
Sharon Bitok Jeptarus,29, alikosa medali pembamba katika mbio za 800m baada ya kuzimaliza katika nafasi ya nne kwa dakika 2:14.16. Alilenga kuimarisha fedha alipata katika mizunguko hiyo miwili mwaka 2022, lakini mambo yakamwendea visivyo.
Rono aliibuka bingwa wa 800m kwa makala ya pili mfululizo kwa 1:53.02 akifuatiwa kwa karibu na Mjapani Kousei Higuchi (1:53.22) na Dalibor Tulak kutoka Jamhuri ya Czech (1:53.33). Brian Kosgei na John Koech walimaliza katika nafasi ya tano na sita, mtawalia.
David Maina, Walter Kalebu, Simon Menza na Paul Simiyu walifuzu kushiriki fainali ya mbio za kupokezana vijiti za 4x100m baada ya kumaliza nusu-fainali yao katika nafasi ya tano kwa sekunde 43.35.
Kenya inatarajiwa kuimarisha nafasi yake nafasi ya tisa inayoshikilia baada ya medali hizo kutoka orodha ya mataifa 78 yanayoshiriki makala hayo ya 25. Ina jumla ya medali 10 (dhahabu nne, fedha nne na shaba mbili). Washindi wa dhahabu watatuzwa Sh3 milioni, fedha Sh2m na shaba Sh1m na serikali.