Ruto kutumia chaguzi ndogo kuwapima nguvu Kindiki, Mudavadi na Wanga
MATOKEO ya chaguzi ndogo za Novemba 27 yatakuwa kipimo kwa Rais William Ruto kuhusu mikakati yake ya kisiasa na muungano atakaobuni katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kufanya vibaya Mbeere Kaskazini, Malava na Kasipul huenda kutasababisha Rais Ruto atafakari kuhusu uwezo wa washirika wake wa sasa.
Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga ni kati ya wanasiasa ambao wataponzwa na Rais iwapo ushindi utakosekana Mbeere Kaskazini, Malava na Kasipul.
Rais Ruto amehepa kampeni za wawaniaji, hatua ambayo wadadisi wanasema ni makusudi katika kupima uzito wa kisiasa wa washirika wake.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema matokeo huenda yakaamua iwapo Profesa Kindiki atadumishwa kama mgombeaji mwenza wa Rais Ruto mnamo 2027.
Nyumbani kwa Profesa Kindiki ni Kaunti ya Tharaka-Nithi umbali wa kilomita 21 pekee kutoka Mbeere Kaskazini.
Kupoteza katika eneo hilo kutadhihirisha kuwa ushawishi wa Rais Ruto umepungua Mlima Kenya ambako alizoa kura nyingi mnamo 2022.
Profesa Kindiki amekuwa mashinani akimpigia kampeni kali mwaniaji wa UDA Leonard Wamuthende.
Mwaniaji huyo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Newton Kariuki maarufu kama Karish wa DP ambaye anaungwa mkono na vinara wengine wa upinzani.
ODM inampa joto Profesa Kindiki baada ya kusisitiza kwamba iwapo itamuunga mkono Rais Ruto, lazima wapewe nafasi ya kuwa mgombeaji mwenza.
Hata hivyo, kwa ODM nako kuna shida huku chama hicho kikitolewa jasho mno eneobunge la Kasipul.
Mgombeaji wa ODM Boyd Were atalazimika kuhimili mawimbi ya Mfanyabiashara Philip Aroko ambaye amepata uungaji mkono kutoka kwa Naibu Gavana Oyugi Magwanga.
Bi Wanga amekuwa akiongoza kampeni za ODM Kasipul na ndiye anategemewa kuhakikisha chama kinadumisha kiti hicho.
Gavana wa zamani wa Migori Okoth Obado na wanasiasa wengine waasi kutoka Luo Nyanza, wamejitokeza na kuwataka raia wamchague Bw Aroko.
Kule Malava, Bw Mudavadi naye lazima ahakikishe David Ndakwa wa UDA anawahi ushindi. Kibarua hicho hata hivyo ni kigumu mno ikizingatiwa vigogo wa upinzani bado wamekita kambi eneobunge hilo kumvumisha Seth Panyako wa DAP-Kenya.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Macharia Munene naye ametabiri kiti cha Mbeere Kaskazini kimeenda na Profesa Kindiki kusalia mgombeaji mwenza wa Rais Ruto kutakuwa ni kupitia hisani tu.
Kuhusu Malava, Bw Macharia anasema itakuwa rahisi kwa Rais Ruto kumpuuza Bw Mudavadi kama mwaniaji wa UDA atashindwa.
“Mudavadi anapigania nafasi yake hata kuliko Profesa Kindiki kwa sababu kulikuwa na mjadala kwamba Raila angechukua nafasi yake kabla ya waziri huyo mkuu kuaga dunia. Profesa Kindiki hana nguzo kisiasa kwa sababu alipewa tu nafasi hiyo baada ya Rigathi Gachagua kuondolewa,” akasema Profesa Macharia.