Habari

Chaguzi ndogo: Sasa katambe

Na WAANDISHI WETU  November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

SASA ni wawaniaji na mungu wao baada ya kampeni za chaguzi ndogo kukamilika Novemba 24, 2025 huku wapigakura wa maeneo hayo wakitarajiwa kuingia debeni Novemba 27,2025.

Chaguzi hizo ndogo zitakuwa zikifanyika maeneobunge ya Ugunja, Kasipul, Magarini, Mbeere Kaskazini na Banisa. Pia kuna uchaguzi mdogo wa Useneta Kaunti ya Baringo.

Aidha kutakuwa na chaguzi nyingine ndogo siku hiyo kwenye wadi 18.

Novemba 23, 2025, Kamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) Alutalala Mukhwana alisema kuwa usalama umeimarishwa hasa katika maeneo ambayo kulikuwa na joto kali wakati wa kampeni.

Bw Mukwana alisema serikali itawatumia maafisa wa usalama waliovalia sare na wale waliovalia kiraia kuhakikisha kuwa usalama upo, wapigakura wanalindwa na hakuna fujo zozote.

“Tunashirikiana na vitengo vyote vya usalama kuhakikisha kwamba chaguzi zinaandaliwa kwa njia ya wazi,” akasema Bw Mukwana akiwa Hola, Kaunti ya Tana River.

“Hakuna nafasi za fujo kwenye chaguzi hizi ndogo na viongozi wanastahili kuelewa kuwa mienendo yao ina athari kwa wafuasi wao,” akaongeza.

Katika chaguzi hizi ndogo macho yatakuwa kwenye maeneobunge ya Mbeere Kaskazini, Malava na Kasipul ambako kuna ushindani mkali kati ya mirengo ya upinzani na serikali.

Mbeere Kaskazini imeshuhudia kampeni kali ambapo pesa zinadaiwa zilimwagwa na mrengo wa serikali huku Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki akikabiliana kwa maneno makali na mtangulizi wake aliyefurushwa afisini Oktoba mwaka jana Rigathi Gachagua.

Profesa Kindiki anamuunga Leonard Muthende wa UDA huku Bw Gachagua naye akivumisha ngoma ya Newton Karish wa DP.

“Ulipewa majukumu kumsaidia Rais kufanya kazi yake lakini ulikuwa ukimtishia na kumchimbia na sasa unawadanganya watu wakufuate kwenye upinzani,” akasema Profesa Kindiki akiwa katika msafara wa kampeni Mbeere Kaskazini mnamo Jumatatu (Novemba 24, 2025).

“Hatuwezi kuenda upinzani ilhali serikali hii sisi ndio tuliichagua na kuna miradi mingi ambayo imepangwa kutekelezwa eneo hili,” akaongeza.

Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na Seneta wa Embu Alexander Mundigi wote wamedai kuwa upinzani unapanga fujo katika uchaguzi huo.

Bw Ruku alidai upinzani umekodisha vijana kutoka Githurai na mitaa mingine Nairobi ambao watawafikishwa Embu kuzua ghasia kisha wenyeji walaumiwe.

Jana, Afisa Mkuu wa IEBC Mbeere Kaskazini John Kinyua alisema kuwa IEBC inapanga kutumia sajili ya kura ya 2022 na si ya 2017 jinsi ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.

“Tutaandaa shughuli ambayo ni ya haki na kusiwe na hofu,” akasema Bw Kinyua.

Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alikuwa amedai kuwa IEBC inalenga kuwafungia wapigakura wengi nje kwa kutumia sajili ya 2017.

Kule Kasipul, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga aliongoza kampeni za mwisho kwa mwaniaji Boyd Were ambaye atakabiliana na Philip Aroko, mgombeaji wa kujitegemea. Wawili hao ndio farasi kwenye kinyángányiro hicho na Bw Aroko amepata uungwaji mkono kutoka kwa Naibu Gavana Oyugi Magwanga na waasi wa ODM.

“Kuonyesha kuwa ODM bado ni dhabiti, tumchague Were ili aendeleze kazi ambayo iliachwa na babake,” akasema Bi Wanga. Bw Boyd ni mwanawe aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Charles Ongóndo ambaye aliuawa Nairobi mnamo Aprili mwaka huu.

Magharibi mwa nchi Seth Panyako wa DAP-Kenya atakuwa akikabiliana na David Ndakwa wa UDA, kwenye uchaguzi ambao umezua hisia kali kati ya upinzani wenyewe kwa wenyewe na pia serikali.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla na Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa wikendi walimpigia debe Bw Ndakwa na kusema ndiye atashirikiana na serikali kukamilisha ndoto ya marehemu mbunge wa eneo hilo Malulu Injendi.

Jana, Bw Mudavadi alihutubia mkutano wa mwisho wa Bw Ndakwa mjini Malava ambako aliwataka wakazi wasimwaibishe kwa sababu ushindi utaonyesha eneo hilo lipo nyuma ya Rais William Ruto mnamo 2027.

“Hii kura ni muhimu kwenu na nawaomba mchague mwenye atafanya kazi na serikali kuwaletea miradi ya maendeleo alivyokuwa akifanya Malulu,” akasema Bw Mudavadi.

Vigogo wa upinzani nao wamekuwa wakiendesha kampeni kali kwa Bw Panyako huku wakisema uchaguzi huo ndio utakuwa ishara kwa Rais Ruto atahudumu kwa muhula moja pekee. Jana waliongoza kampeni ya mwisho ya Bw Panyako maeneo mbalimbali Malava.