Habari

Afueni kwa wakazi wa Makongeni mahakama ikisimamisha kwa muda shughuli ya ubomoaji

Na JOSEPH WANGUI November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa mtaa wa Makongeni jijini Nairobi wamewasilisha kesi katika Mahakama Kuu kupinga mchakato unaoendelea wa kuwafurusha kupisha mradi wa serikali wa makazi nafuu, wakidai kuwa haki zao za msingi zimekiukwa kwa njia nyingi.

Wakazi hao Brian Riang’a, Daniel Ndiau Okul, na Joshua Chuma, waliwasilisha kesi hiyo kwa niaba ya wakazi waathiriwa, wakishtaki Bodi ya Nyumba za Gharama Nafuu, Wizara ya Ardhi, Ujenzi, Makazi na Maendeleo ya Miji, na mashirika mengine ya serikali kwa kukiuka matakwa ya kikatiba katika mipango yao ya kuwahamisha wakazi.

Suala kuu kwenye kesi hiyo ni umiliki wa ardhi inayozozaniwa, ambayo ni mali ya Hazina ya Wafanyakazi Wastaafu wa Shirika la Reli la Kenya chini ya makubaliano maalum na Shirika la Reli Kenya.

Ingawa shirika hilo lina hati halali ya umiliki, wakazi wanadai kuwa mchakato wa kupata fidia ya wakazi kuhusu ubomoaji haijakuwa wazi na pia ni wa kulazimisha.

Katika kiapo chake, Bw Riang’a, ambaye ni wakili, anadai kuwa wakazi wengi, hasa wasiojua kusoma na kuandika, walisaini nyaraka bila kuelewa kilichomo, jambo linalodhoofisha fidia ya kueleweka na kukiuka Ibara ya 35 kuhusu haki ya kupata taarifa.

Inasemekana kuwa wakazi walipatiwa Sh150,000 kama fidia na kuahidiwa kupewa kipaumbele katika mgao wa nyumba mpya zitakazojengwa.

Hata hivyo, ombi hilo linadai kuwa kiasi hicho hakitoshi kupata makazi mbadala katika soko la nyumba za kupanga jijini Nairobi ambalo lina bei ya juu.

Notisi ya miezi mitatu ya kuwafukuza pia imetajwa kuwa fupi kupita kiasi, ikidaiwa kukiuka Ibara ya 43(1)(b) kuhusu haki ya makazi yanayofikika na Ibara ya 28 kuhusu heshima ya utu.

Ombi hilo pia linahoji ukamilifu wa ushirikishwaji wa umma.

Licha ya madai ya serikali kuwa mashauriano yalifanyika, wakazi wanasema vikao hivyo vilikuwa vya kibaguzi na havikuwahusisha wakazi wote walioathiriwa, hivyo kukosa kutimiza matakwa ya ushiriki wa umma chini ya Ibara ya 10.

Pia wanasema kuwa hakuna hakikisho lililoandikwa kuhusu kile wanachopatia kipaumbele katika kupata nyumba mpya, jambo linaloongeza hofu ya kufurushwa bila suluhu.

Waliojumuishwa kama walioshtakiwa ni watano: Bodi ya Makazi Nafuu, Katibu Mkuu na Waziri wa Makazi, Hazina ya Wastaafu wa Shirika la Reli, na Mwanasheria Mkuu. Wakazi hao wanatafuta tamko kuwa haki zao zimekiukwa, maagizo ya kupewa fidia inayolingana na thamani ya nyumba mpya, na maagizo ya kufanywa kwa ushirikishaji sahihi wa umma kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.

Kesi hiyo inaongeza uzito kwa wasiwasi mpana kuhusu mpango wa makazi nafuu nchini Kenya, ambao umekumbwa na madai ya kufurushwa kwa nguvu, fidia duni, na ukosefu wa uwazi.

Uamuzi unaowapendelea wakazi wa Makongeni unaweza kuweka miondoko muhimu kuhusu wajibu wa serikali kwa jamii zinazohamishwa. Mkutano wa kusimamia mwenendo wa kesi umepangwa kufanyika kesho.