Pigo jingine kwa familia ya Raila dada yake akifariki akitibiwa hospitalini
FAMILIA pana ya aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Raila Odinga, imepata pigo jingine kufuatia kifo cha dadake Beryl Achieng Odinga.
Kifo cha Achieng kilitangazwa na dada yao mdogo, Ruth Odinga, ambaye alisema kuwa Beryl alifariki Jumanne, Novemba 25.
Hata hivyo, hakufichua chanzo cha kifo hicho.
“Ni kwa moyo mzito lakini tukikubali mapenzi ya Mungu, tunatangaza kifo cha ghafla cha Beryl Achieng Odinga. Binti wa marehemu Jaramogi Oginga Odinga na Mama Mary Ajuma Oginga. Mama yake Ami Auma, Chizi na Taurus,” Ruth alitangaza.
“Ingawa tumehuzunishwa sana na kifo chake na pengo kubwa aliloliacha maishani mwetu, tunapata faraja tukiamini yuko salama mikononi mwa Bwana, na tunashukuru kwa zawadi ya muda tuliojaaliwa kushiriki naye,” aliongeza.
Beryl alikuwa dada yake Seneta Oburu Oginga, Raila Odinga, Akinyi Wenwa, na Ruth Odinga, miongoni mwa wengine.
Alikuwa Shemeji ya Dkt Anne Oburu, Dkt Canon Ida Odinga, Tabu Osewe na Judy Oburu.
“Ingawa tumegubikwa na huzuni kuu kutokana na kifo chake na pengo kubwa aliloacha maishani mwetu, tunapata faraja kwa kuamini kuwa sasa yuko salama mikononi mwa Bwana. Tunashukuru kwa zawadi ya muda tuliobarikiwa kuwa naye na kwa mchango mkubwa na wa kipekee aliokuwa nao kwa wote waliomfahamu,” alisema Ruth.