Jinsi maradhi yasiyo ya kuambukiza yanalemea vijana kutoka familia za pato la chini
KWA miaka 13, Elizabeth Nyawira Muriithi, amekuwa akiishi na maradhi ya kisukari aina ya type 1.
“Nilianza kwa kuhisi kiu kisichokoma, ambapo ningeweza kunywa kufikia lita nane za maji kwa siku, na bado nisitosheke. Hali hii iliandamana na hisia za kuenda haja ndogo mara kwa mara, kutamani vitu vitamu kama soda na biskuti, na baadaye nilianza kutapika,” asema.
Wazazi wake walimpeleka kutoka kituo kimoja cha afya hadi kingine, mara akidhaniwa kuwa alikuwa anaugua malaria. Hali hii iliendelea hadi wakati mmoja alipozimia na kupoteza fahamu kutokana na kiwango cha juu cha sukari.
“Nilipelekwa katika Hospitali ya St Francis Kasarani, ambapo kiwango cha sukari kwenye damu kiligundulika kuwa cha juu zaidi, na hapo ndipo madaktari walipogundua kuwa nilikuwa naugua kisukari,” aeleza.
Simulizi ya Nyawira inaakisi taswira ambayo imeendelea kushuhudiwa ambapo idadi ya vijana wanaougua maradhi yasiyoambukiza kama vile kisukari, saratani, pumu na shinikizo la damu, inazidi kuongezeka hasa barani Afrika.
“Tunashuhudia ongezeko la maradhi haya huku mifumo yetu ya afya ikibaki kushughulikia tu magonjwa yanayoambukiza,” asema Dkt Catherine Karekezi, Mkurugenzi Mtendaji wa muungano wa mashirika yanayohusika na maradhi yasiyoambukizika nchini, NCD-K Alliance.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanawakilisha zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa waliolazwa hospitalini, na asilimia 40 ya vifo vinavyotokea hospitali nchini Kenya.
Aidha, ripoti zaidi zinaonyesha kuwa asilimia 22 ya vifo vyote vinavyotokea miongoni mwa watu kabla ya kutimu umri wa miaka 40, husababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na majeraha.
Miongoni mwa vijana walio chini ya umri wa miaka 40, maradhi ya kisukari aina ya type 2, vile vile aina nyingine za kisukari, zimeorodheshwa nambari mbili miongoni mwa maradhi hatari yasiyo ya kuambukiza.
Ingawa takwimu za kuenea kwa maradhi ya kisukari kwa misingi ya umri bado ni chache, wataalam wanasema kwamba ushahidi unazidi kuongezeka kuashiria kuwa ugonjwa huu unaendelea kuathiri vijana nchini, huku yakichochewa na mabadiliko ya mtindo wa maisha, lishe duni, na kupungua kwa shughuli za kimwili.
Kulingana na wataalamu, watoto na vijana wanaoishi na hali hii kwa muda mrefu, mara nyingi hukabiliwa na matatizo kama vile kushindwa kufikia huduma za matibabu, hasa katika vituo vya afya vya umma.
Kulingana na Parth Narendran, Profesa wa tiba ya kisukari na mshauri katika Chuo Kikuu cha Birmingham, nchini Uingereza, changamoto kuu ni kwamba mara nyingi maradhi ya kisukari aina ya type 1 hujitokeza wakati tayari kuna tatizo lingine la kiafya, ambapo ni rahisi kwa watu kudhani kuwa ni ugonjwa mwingine.
Changamoto kuu kwa wagonjwa, ni matatizo ya kiafya yanayoambatana na hali hii.
“Mara nyingi mimi huhisi uchovu hasa kutokana na kujidunga sindano kila mara. Pia kuna vikwazo vya lishe ambapo lazima utilie maanani unachotia mdomoni,” aeleza Nyawira.
Tatizo hili, pamoja na gharama kubwa za matibabu, inamaanisha kuwa kwa vijana wengi, hasa wale kutoka jamii maskini au vijijini, wanashindwa kudhibiti maradhi haya.
Nyawira anaelewa vyema hali hiyo kwani baada ya kutimu umri wa miaka 25, aliondolewa katika mpango ambao awali ulikuwa unamhakikishia insulini na vifaa vya uchunguzi bila malipo.
Na hivyo, bila ajira, sasa analazimika kukabiliana na gharama za matibabu.
“Kichupa kimoja cha insulini kinagharimu takriban Sh2,000, na ninahitaji kadhaa kila mwezi. Kwa upande mwingine, kwa kila pakiti ya vishale 50 vya kupima kiwango cha sukari kwenye damu, nalazimika kulipia Sh1,200, na napima mara kadhaa kwa siku.”
Kulingana na Dkt Jeremiah Nganda, mtafiti wa mifumo ya afya katika kituo cha Center, Chuo Kikuu cha Strathmore, baadhi ya changamoto hizi ni kutokana na kuwa Kenya haina sera ya kitaifa inayolenga hasa magonjwa ya muda mrefu miongoni mwa vijana.
Kutokuwepo kwa sera zinazolenga vijana, Dkt Nganda asema, kunamaanisha kwamba, hata pale ushahidi unaonyesha mzigo wa magonjwa unawaathiri vijana zaidi, hakuna hatua maalumu au programu zinazolenga hali hii.
“Hii inamaanisha kuwa, jitihada za kuzuia, kusimamia, na kutibu magonjwa haya huenda zisipewe kipaumbele kama inavyostahili.”
Kulingana na Dkt Nganda, baadhi ya kaunti, kama vile Kisumu, zimeshajaribu kuandaa sera za afya kwa vijana, lakini asema kuwa kuwepo kwa hati za sera pekee haitoshi, na badala yake, mkazo unapaswa kuwa katika utekelezaji.
Zaidi ya hayo, anafafanua kuwa Kenya inaendelea kukabili changamoto za upungufu wa sera na utekelezaji dhaifu.
“Baadhi ya hati za sera za aina hii zimepitwa na wakati pasipo kusasishwa, huku nyingine zikibaki kutotekelezwa.”
Hivyo basi, asema, kuna haja ya sera za kisasa, zenye ushahidi, na zinazoambatana na mzigo wa magonjwa, vile vile tabia za kisasa miongoni mwa vijana hasa katika masuala ya huduma za afya.