Kenya kuwa mwenyeji wa Raga za Dunia za Sevens Februari 2026
KENYA imechaguliwa kuwa mwenyeji wa duru moja ya mashindano ya dunia ya raga ya wachezaji saba kila upande ya daraja la pili (HSBC Division 2).
Duru hiyo itaandaliwa ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Februari 14-15, 2026. Timu zote za Kenya – Shujaa (wanaume) na Lionesses (wanawake) – zitashiriki mashindano hayo. Kenya imekuwa ikijaribu kuwa mwenyeji kwa karibu miaka 10.
“Shirikisho la Raga Duniani (World Rugby) liliangalia uwezo wa Kenya kuandaa mashindano makubwa. Liliridhishwa kuwa tumeshawahi kuwa wenyeji wa mashindano ya dunia ya chipukizi mwaka 2009 na pia mwaka 2023 pamoja na Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande ambalo tuliandaa Novemba 15-16,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Raga Kenya (KRU), Thomas Odundo ameeleza Taifa Leo, Jumatano.
Mbali na kuwa Kenya imeandaa mashindano hayo makubwa, Odundo anasema kuwa World Rugby pia ilifurahia hoteli nyingi za kisasa za timu kuishi, uwanja mzuri wa mashindano pamoja na ufuasi mkubwa wa mashabiki.
Kenya ilituma ombi lake la kutaka kuwa mwenyeji mara tu World Rugby iliitisha mataifa kuwania uenyeji wa duru hizo Juni 2025.
Mkurugenzi wa Mashindano wa World Rugby, Nigel Cass alizuru Nairobi hapo Novemba 14 na kukagua viwanja vya Nyayo na Talanta City.
Duru nyingine za ligi hiyo zitaandaliwa katika miji ya Montevideo (Uruguay) na Sao Paulo (Brazil). Kila duru itahusisha mataifa sita ya wanaume na pia sita ya wanawake.
Timu nne-bora baada ya duru hizo tatu kusakatwa zitaingia mashindano ya dunia kuchapana na nne za mwisho kutoka ligi ya daraja la juu kabisa (HSBC SVNS Series) ili kuamua timu nne zitakazoshiriki ligi ya daraja la juu kabisa msimu 2026-2027.
Shujaa ilikamilisha Kombe la Afrika la Wanaume katika nafasi ya tatu mwezi Juni nchini Mauritius nayo Lionesses ikakamata nafasi ya pili katika Kombe la Afrika la Wanawake ugani RFUEA jijini Nairobi hapo Novemba 15-16.
Matokeo yao yanamaanisha kuwa wenyeji Kenya watalazimika kujituma zaidi ya kawaida mbele ya mashabiki wao ugani Nyayo pamoja na mijini Montevideo na Sao Paulo ili kukamilisha daraja la pili ndani ya nne-bora.