Oburu kukatiza likizo yake Dubai kupanga mazishi ya dadake
KIONGOZI wa chama cha ODM, Dkt Oburu Oginga anatarajiwa kurejea nchini Ijumaa, akikatiza mapumziko yake mafupi ili achukue tena jukumu zito la kuongoza familia ya baba yake katika kipindi kingine cha majonzi kufuatia kifo cha dada yao Beryl Achieng’ Odinga, aliyefariki Jumanne.
Dkt Oburu ambaye ni msemaji wa familia hiyo aliondoka nchini Novemba 21 kuelekea Dubai kwa mapumziko, ambayo dada yake, Bi Ruth Odinga, alisema yalikuwa ya kupunguza uchovu wa kipindi kirefu cha kisiasa kilichojaa misukosuko na msongo wa hisia.
Hata hivyo, tangu kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga mnamo Oktoba 15, 2025, familia hiyo haijapata nafasi ya kupumua. Kila siku imekuwa ni mfululizo wa wageni, viongozi, wafuasi na marafiki wanaoendelea kufurika katika mashamba ya Opoda na Kang’o ka Jaramogi kutoa pole zao.
Kifo cha Bi Achieng’ kimeongeza giza katika kipindi hiki kigumu, kikizidisha uchungu wa familia na kugeuza majonzi ya awali kuwa msiba maradufu ulioshtua mno jamaa na marafiki wao.
Marafiki na jamaa wamekuwa wakifika katika hifadhi ya maiti ya Lee kuutazama mwili huku wengine wakifika nyumbani kwake Kileleshwa kutoa rambirambi.
Akizungumza na Taifa Leo kwa simu, dada wa kambo wa marehemu, Bi Emily Oginga, alisema wanasubiri kurejea kwa kiongozi wa familia ili kuanza mipango ya mazishi.
“Si rahisi kwetu; ni kama msimu wa mavuno ya vifo umeingia kwetu. Tunasubiri Dkt Oburu ambaye anatarajiwa kuwasili Ijumaa ili tuanze mikutano ya kupanga mazishi ya dada yetu. Kwa sasa marafiki na jamaa wanaendelea kutoa pole nyumbani kwake Kileleshwa,” alisema Emily.
Aliongeza kuwa wengine pia wanatembelea Kang’o ka Jaramogi kutoa pole kwa Bi Betty Oginga na Bi Susan Oginga, waliofiwa tena ndani ya muda wa miezi miwili.
Kulingana na Bw Jaoko Oburu, mwanawe Dkt Oginga, kifo cha shangazi yake kimemgusa sana kwani amepoteza mtu aliyekuwa karibu naye.
“Kwa mama yetu mpendwa na mlezi wetu Aunty B, maneno hayawezi kueleza huzuni ya kukupoteza siku 40 tu baada ya kumpoteza mlezi mwingine, Baba. Utakumbukwa sana. Tutakupenda daima na kukuenzi,” alisema Jaoko.
Alisema familia ililemewa na majonzi katika wiki zilizopita, hali iliyowalazimu kumshinikiza baba yao apumzike baada ya ratiba nzito iliyomnyima muda wa kuomboleza kakake.
Familia hiyo pia imekuwa ikihudhuria shughuli nyingi za chama bila nafasi ya kiongozi huyo wa ODM mwenye umri wa miaka 82 muda wa kupumzika.
“Tumehudhuria shughuli nyingi Homa Bay, Migori na hata maadhimisho ya ODM@20. Tukagundua kuwa kiongozi wa chama hakuwa amepata hata dakika ya kuomboleza ndugu yake. Ndiyo maana tulisisitiza apate mapumziko, ambayo alichukua Alhamisi iliyopita Dubai,” alisema.
Kwa bahati mbaya, msiba mwingine umepata familia kufuatia kifo cha Bi Achieng’.