Habari za Kitaifa

Chaguzi ndogo: Upigaji kura waendelea IEBC ikitoa hakikisho

Na BENSON MATHEKA November 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Upigaji kura unaendelea katika chaguzi ndogo 24 huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ikiwahakikishia wapiga kura kuwa zoezi hilo litaendelea bila madhara licha ya taarifa za kuchelewa kuanza kwa katika baadhi ya maeneo, ikisema muda uliopotea utafidiwa ili kuhakikisha kila mpiga kura anapata nafasi ya kupiga kura.

Tume hiyo ilitoa ufafanuzi huo mapema Alhamisi, muda mfupi baada ya upigaji kura kuanza katika vituo mbalimbali nchini katika chaguzi ndogo zinazoendelea.

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X Alhamisi, Novemba 27, 2025, IEBC ilisema upigaji kura ulianza rasmi alfajiri.

“Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na vitafungwa saa kumi na moja jioni,” imesema taarifa ya IEBC.

IEBC ilifafanua kuwa ingawa muda rasmi wa kufunga vituo ni saa kumi na moja jioni, hakuna mpiga kura atakayezuiwa kupiga kura kutokana na ucheleweshaji uliochangiwa na changamoto za kiufundi, utendaji au vifaa. Tume hiyo ilisema dakika zozote zitakazopotea zitafidiwa ili kuhakikisha mchakato unasalia huru, wa haki na wa kuaminika.

“Dakika zozote zitakazopotea wakati wa upigaji kura zitafidiwa wakati wa kufunga kituo, na wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni saa kumi na moja jioni wataruhusiwa kupiga kura,” taarifa hiyo iliongeza.

Ufafanuzi huo unajiri kukiwa na ripoti za hitilafu ndogo katika baadhi ya vituo, ikiwemo kuchelewa kwa vifaa vya kutambua wapiga kura. IEBC ilisema lengo ni kutuliza hofu miongoni mwa wananchi waliokuwa wanaogopa kukosa nafasi ya kushiriki uchaguzi kwa kucheleweshwa kwa njia moja au nyingine.

Katika maeneo mbalimbali nchini, wapiga kura walianza kujitokeza kuanzia saa kumi na mbili asubuhi, wengine wakifika kabla ya alfajiri kuepuka foleni ndefu. Waangalizi walisema hali ilikuwa shwari, huku ulinzi ukiimarishwa kuhakikisha utulivu.

IEBC ilisisitiza kuwa maafisa wake wameelekezwa kuhesabu muda uliopotea, hasa katika vituo vilivyoanza kupiga kura kwa kuchelewa.

Tume hiyo pia iliwakumbusha Wakenya kuwa sheria inawapa haki ya kupiga kura wale wote watakaokuwa kwenye foleni kufikia saa kumi na moja jioni, na kuwataka kudumisha utulivu na subira.

IEBC imesema itaendelea kufuatilia hali katika vituo vyote na kutoa taarifa inapohitajika, ikiwahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa amani.