• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Mashine za kukama maziwa zabadili taswira ya ufugaji

AKILIMALI: Mashine za kukama maziwa zabadili taswira ya ufugaji

Na SAMMY WAWERU

MWAKA 2018, Rais Uhuru Kenyatta alihimiza wakulima na wafugaji kutilia maanani vigezo vya kisasa katika kilimo, akihoji kuwa vitaimarisha utendakazi wa uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Akihutubu Desemba 5 katika ufungaji wa maonyesho ya mifugo kaunti ya Narok, Rais alisema soko la sasa la bidhaa za kilimo lina ushindani mkuu na kwamba linahitaji bidhaa zilizozingatia ubora. Alisema ubora wa mazao ndio utaimarisha soko la bidhaa zinazozalishwa humu nchini.

Akisisitizia kuhusu uzalishaji wa maziwa Bw Kenyatta aliwataka wakulima kuimarisha ng’ombe wanaofuga hasa kwa kukumbatia mfumo wa mbegu za kisasa katika utungishaji wa ujauzito, uhamilishaji maarufu AI.

Aidha, alisema mfumo wa kisasa wa kujamiisha mifugo umezingatia ubora wa mazao yanayohitajika si tu katika soko la ndani kwa ndani, ila la kimataifa na lenye bei bora.

“Sioni haja ya kusema mimi nina ng’ombe elfu moja au mbili wenye ubora na mazao duni ambao nikiuza watanipa pesa kidogo. Ni heri niwe na ng’ombe mmoja au wawili nitakaowauza kwa bei bora. Tuzingatie ubora wa kilimo, na hatuna budi ila kuuimarisha kwa kuzingatia mifumo ya kisasa,” alieleza Rais Kenyatta.

Ng’ombe hufugwa kwa minajili ya maziwa na nyama, ngozi yake ikitumiwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa kama viatu, mapochi, magoma, mishipi na hata mavazi kwa baadhi ya jamii zikitumbuiza kuonesha itikadi, mila na tamaduni zake. Miongoni mwa ajenda kuu nne za Rais Kenyatta, ni usalama wa chakula nchini.

Katika makazi tulivu na ya kifahari kilomita chache kutoka mji wa Ongata Rongai, kaunti ya Kajiado, Bi Agnes Omingo anafahamu fika tija za kukumbatia mfumo wa kisasa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Ni mwendo wa saa tano na nusu hivi za asubuhi, Akilimali inatua kwa mama huyu, ambaye ni mkwasi wa ukarimu.

Tunampata katika chumba maalumu cha kukama ng’ombe akiwa na wafanyakazi kadhaa, na hapa shughuli za usafi zimeshika kasi. Si usafi wa madoo ya kukama kwa mikono, ila ni ya mashine za kisasa zinazotumika kuendesha shughuli ya kupata maziwa kutoka kwa ng’ombe. Mashine zenyewe hutumia nguvu za umeme kukama. Kwa jumla ni 10, na zimesindikwa na kupangwa kwa makundi mawili mawili.

Kila doo la glesi linalositiri maziwa katika mashine hizo, linasuguliwa ndani kwa kifaa maalumu ingawa Agnes anasema wakati mwingine hutumia stima kuzing’arisha. Kulingana na meneja wake Andrew Tuitoek, usafi wa hadhi ya juu ndio mwanzo wa ufanisi katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. “Usuguaji wa madoo ya mashine hizi huufanya mara moja kwa wiki. Hatua ya kwanza kuyakamua ni kwa maji baridi, kisha moto yenye joto la kati ya nyuzi 70-80 sentigredi. Tunakamilisha kwa maji baridi,” afafanua Bw Tuitoek.

Ng’ombe wa Agnes hukamwa mara tatu kwa siku; alfajiri, adhuhuri-saa sita na majira ya jioni-saa mbili. Kila baada ya kukama, madoo sharti yaoshwe. Awali kabla ya kuanza kutumia mfumo wa kisasa, ilichukua zaidi ya saa tatu kufanya shughuli ya ukamaji. Kwa kutumia mashine, mfugaji huyu anadokeza kwamba muda huo umepungua hadi chini ya saa moja, kukama ng’ombe 33 alionao wa maziwa. “Mashine hizi huuzwa kwa pea, kila kipande kikikama mmoja. Kwa muda wa dakika 7 pekee hukama ng’ombe 10 kwa wakati mmoja. Kitambo, wafanyakazi waliishi kulalamikia machovu kwa sababu walikuwa wakiamka saa tisa za usiku,” aelezea Bi Agnes.

Agnes Omingo, tayari kuwatilia ng’ombe wake chakula. Picha/ Sammy Waweru

Ni kupitia utafiti aliofanya kwenye mitandao akagundua Uholanzi imestaarabika, kwa kuvumbua mashine zinazorahisha kazi ya kukama ng’ombe. “Niliandamana na mzee wangu (akimaanisha mume) hadi Uholanzi kwa kutumia anwani tulizopata, na ndipo tulinunua mitambo hii,” anasema. Anaongeza kusema kuwa kampuni iliyowauzia mashine hizo, waliafikiana kufungua duka la kuziuza ili kupevusha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini. “Zinapopata hitilafu, hurekebishiwa katika duka lijulikanalo kama Euro Dairy Shop, ambalo lina wataalamu na vifaa. Pia, huuza mashine hizi,” alisema wakati wa mahojiano, japo hakufichua bei yake.

Katika chumba cha kukama, ameziunganisha na jokofu ambapo maziwa huelekezwa humo kwa minajili ya kuyahifadhi kwa muda. Sawa na eneo hilo, makazi ya ng’ombe kupumzika, kula, kunywa maji na kulala, yana redio. “Redio hizi si za kutumbuiza watu, ila ni ng’ombe,” akasema mfanyakazi mmoja, Bi Agnes akifafanua kwamba huwaongoa na kuwatuliza “hasa wakati wa kuwakama, ili kuondoa mzongo za mawazo”.

Wamegawanywa kwa kundi la wanaokamwa na ndama, kila kundi likiwa na zizi lake. La kutia moyo, kila ng’ombe ana sehemu yake ya kulala na yenye godoro maalum.

Agnes alianza ufugaji wa ng’ombe mnamo 1991.

“Nilianza kwa ng’ombe wawili pekee wa maziwa ya familia yangu,” asema. Anafichua kwamba alikuwa mhasibu wa benki moja nchini, na kwa sababu alipenda ufugaji kama mama halisi wa Kiafrika aligura kazi hiyo mwaka wa 1997 ili kuuvalia njuga kikamilifu. Mwaka wa 2010, alinunua ng’ombe watatu wa maziwa aina ya Friesian, kutoka Rift Valley Institute, RVI, taasisi tajika nchini katika mafunzo ya ufugaji na kilimo, mmoja akigharimu Sh150,000.

Anasema ng’ombe hao ndio wamezaana hadi kufikia kiwango alichonacho kwa sasa. Ili kuwatunga uja uzito, hununua mbegu za kisasa aina ya AI, kutoka Marekani au Uholanzi, ambapo hujamiishwa kwa kutumia nguvu za umeme.

“AI hizo ni karibu asilimia 100 hakikisho utapata jinsia unayonuwia,” aeleza Bi Agnes.

Hufuga ng’ombe wa kike pekee kwa madhumuni ya uzalishaji wa maziwa, akisema wa kiume azaliwapo humuuza.

Baadhi ya kaunti nchini zimeanza kutoa huduma za AI kwa wafugaji wa ng’ombe bila malipo ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa muhimu ya maziwa.

Marekani na Uholanzi ni miongoni mwa mataifa tajika duniani katika ufugaji wa ng’ombe za maziwa kwa mfumo wa kileo.

You can share this post!

Eliud Ndung’u Kinuthia: Rais amependekeza bunge...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu zinazodhihirisha...

adminleo