Chaguzi ndogo: Madai ya maajenti kuhangaishwa yaibuka
Madai ya maajenti wa wagombeaji kushambuliwa na kuhangaishwa yameibuka katika chaguzi ndogo hasa eneo la Mbeere Kaskazini kaunti ya Embu na Magarini kaunti ya Kilifi. Polisi wameweka kizuizi katika baadhi ya barabara eneo la Kasipul kaunti ya Homa Bay.
Kiongozi wa Chama Cha Kazi (CCK) Moses Kuria alidai kuwa maajenti wa vyama waliokuwa wakielekea vituoni walishambuliwa.
Kuria alitoa madai hayo kupitia mtandao wa X, akisema wahuni walivamia maajenti waliokuwa safarini kwenda vituo mbalimbali wakati zoezi la upigaji kura likianza.
Alitoa kauli yake huku serikali na upinzani zikirushiana lawama wiki nzima kuhusu madai ya njama za kuvuruga uchaguzi huo. Hizi ni chaguzi ndogo zenye ushindani mkali zaidi nchini mwaka huu, na zimevutia uangalizi wa karibu kutoka kwa viongozi wa kisiasa na waangalizi wa uchaguzi.
Siku ya Jumatano, chama tawala UDA kilimlaumu upinzani kwa kupanga vurugu Mbeere Kaskazini. Mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire alidai makundi fulani kutoka upinzani yalikuwa yamewasafirisha watu kuingia eneo hilo ili kuzua taharuki na kuvuruga upigaji kura.
Hata hivyo, upinzani ulipinga vikali madai hayo, na badala yake ukalaumu serikali kwa kupanga wizi wa kura kupitia kuingiza mkaratasi bandia. Jumatano usiku, viongozi wa upinzani—Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua na Eugene Wamalwa—walidai kuwepo njama kubwa ya kufanikisha wizi huo.
Wakati huohuo, Huduma ya Polisi nchini ilitoa onyo dhidi ya jitihada zozote za kuvuruga uchaguzi, ikisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote 24 yanayofanya uchaguzi huo. Polisi waliwataka wanasiasa kuepuka kuchochea wafuasi wao.
Katika Magarini, Kaunti ya Kilifi, mgombeaji wa ODM Harrison Kombe alieleza kutoridhishwa baada ya ajenti wake kutolewa nje ya chumba cha kupigia kura katika Kituo cha Mjanaheri.