Ni kunoma: Kaluma apigwa kichwani, Panyako abubujikwa machozi diwani wa zamani akivamiwa
MBUNGE wa Homa Bay Town, Peter Kaluma, na mlinzi wake walijeruhiwa Novemba 27, 2025, baada ya kushambuliwa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kasipul.
Aidha, ripoti zinasema kuwa bunduki ya mlinzi wake ilipotea katika tukio hilo.
Akizungumza akiwa amelowa damu usoni, Kaluma alidai kushambuliwa na mgombea huru Philip Aroko pamoja na kundi la wahuni.
“Nimevamiwa na Aroko na kundi lake. Wameenda na bunduki ya mlinzi wangu. Lakini niko hapa kusubiri mgombea wetu wa ODM apige kura. Hakuna cha kuogopa. Watu wajitokeze wapige kura,” Kaluma alisema.
Alitoa wito kwa wakazi wa Kasipul kutotishwa na vurugu hizo, akisema lengo la wahuni ni kuwatisha wapiga kura.
“Watu wasipigane. Mkivamiwa, msijibu. Nimevamiwa lakini nipo hapa. Njooni mpige kura.”
Mapema leo katika Shule ya Msingi ya Agoro Sare, Kaluma aliambia wanahabari kwamba idadi ya wapiga kura ilikuwa ya chini, lakini ni jambo la kawaida katika uchaguzi mdogo.
“Hii ni kawaida. Baadaye kuanzia saa tano hadi saa saba idadi huongezeka,” alisema.
Vurugu katika Kasipul zinalingana na hekaheka zinazoshuhudiwa Malava, ambako mgombea wa DAP–K, Seth Panyako, alibubujika machozi wakati wa kupiga kura kutokana na kile alichotaja kuwa vitisho dhidi ya maisha yake, kuvamiwa hotelini na njama za kuingilia uchaguzi.
Panyako, akiongea akiwa na kiongozi wa DAP–K Eugene Wamalwa, alidai maafisa wa usalama walishirikiana na wahalifu kumlenga yeye na mkewe.
“Nilipata taarifa kuwa hoteli yetu ingevamiwa, sikujua ilikuwa kweli hadi walipofika. Serikali kupitia watu fulani walipewa maagizo kuniua. Hakuna njia nyingine ya kumfanya mgombeaji wao ashinde,” alisema huku akilia.
Alisema hoteli ya Downhill Hotel, ilivamiwa na askari na watu aliowaita wahalifu, wakilenga chumba chake, magari yake na ukumbi aliotaka kutumia kama kituo chake cha kujumuisha matokeo.
Wamalwa alidai kuwa magari ya polisi kutoka Kituo cha Matete ndiyo yalivunja lango na kwamba Panyako alilazimika kutoroka kwa pikipiki.
Huko Mbeere North, kiongozi wa Chama Cha Kazi (CCK), Moses Kuria, alidai kuwa maajenti wake walivamiwa wakielekea vituoni mapema asubuhi.
Katika uchaguzi mdogo unaoendelea katika wadi ya Mumbuni North, Kaunti ya Machakos, aliyekuwa Mwakilishi wa Wadi (MCA) Paul Museku alishambuliwa baada ya kufika kituo cha kupigia kura. Watu wanaodaiwa kuwa wakazi wa eneo hilo walimvamia mara moja, wakimlaumu kwa kujaribu kuhonga wapiga kura.
Tukio hilo lilitokea alipokuwa akielekea katika kituo cha kupigia kura cha Mung’ala.
Polisi waliingilia kati na kumuokoa Museku.