Makala

Hofu visa vya wavulana kudhulumiwa jandoni hadi kufa vikiongezeka

Na MERCY KOSKEI November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VISA vya wavulana waliotahiriwa kujeruhiwa au hata kufa kwa madai ya kudhulumiwa na walezi wao katika vituo mbalimbali vimeongezekana katika Kaunti ya Nakuru.

Katika kisa kimoja, mvulana mmoja alikufa wiki hii na wengine wawili wakajeruhiwa vibaya baada ya kutahiriwa katika hospitali moja mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Visa hivyo vimeibua hofu kuhusu usalama wa watoto hao wanaotengwa kwa ajili ya kutunzwa baada ya kutahiriwa.

Mnamo Novemba 21, wavulana wawili wenye umri wa miaka 14 na 15 walidaiwa kudhulumiwa na walezi katika kitongoji duni cha KCC waliripotiwa kupata afueni.

Wavulana hao walikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha na sasa wanapata afueni.

Kaka hao wa Naivasha waliambia Taifa Leo kwamba walivumilia dhuluma, mateso na kichapo kutoka kwa mlezi wao- ambaye alitwikwa jukumu la kuelekeza wakiendelea kupona na kuwafundisha maadili.

Baba ya waathiriwa, Peter (sio jina lake halisi) alisema alikodisha chumba kidogo karibu na nyumba yake kitumike kuwatunza wavulana hao baada ya kutahiriwa mnamo Novemba 11.

Mwana wa jirani wao alijitolea kuwatunza lakini baadaye aliwalete vijana wengi na hivyo kugeuza eneo hilo kuwa kituo cha mateso.

Peter anasema hakutembelea chumba hicho ambako wavulana wake walikuwa wakitunzwa-kutokana na sababu za kitamaduni-hadi Novemba 21 alipohisi kwamba hali haikuwa shwari.

“Nilipowauliza, walilia wakiniambia wamekuwa wakipigwa kila siku na zaidi ya wanaume watano,” akasema.

“Mdogo kati ya wavulana hao hangeweza kuketi vizuri wala kutembea vizuri. Aidha, alikuwa na majeraha mgongoni na miguuni. Yule mwenye umri mkubwa pia alikuwa amejeruhiwa vibaya,” akaongeza.

Polisi walisema wameanzisha uchunguzi kwa lengo la kuwakamatwa washukiwa, ambao inasemekana kuwa walitoroka.

Katika kijiji cha Keriko Central, kaunti ndogo ya Bahati, mvulana wa Gredi 9 alikufa kutokana na majeraha aliyodaiwa kupata baada ya kudhulumiwa na walezi.

Amos Ng’ang’a, afisa wa Nyumba Kumi alisema alipata habari kuhusu kifo cha mvulana huyo kutoka kwa watu wa familia yake walipokuwa wakisaka gari la kupeleka maiti yake katika mochari.

Bw Ng’ang’a aliwasilisha ripoti kwa kituo cha polisi cha Bahati na maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Mwendazake, ambaye amekuwa akiishi na babu yake, ameishi katika kituo cha malezi kwa wiki tatu.

Ripoti ya upasuaji iliyofanyika katika hifadhi ya maiti ya Nakuru City ilifichua kuwa mvulana huyo alikufa baada ya kufuja damu ndani ya mwili baada ya kushambuliwa.