Makala

Maxine alikuwa na ndoa ya vurugu na ukorofi

Na RICHARD MUNGUTI November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

DEREVA wa magari ya Safari Rally, Maxine Wahome alikuwa akinyanyaswa na mumewe marehemu Asad Khan, Mahakama kuu iliambiwa Jumatano.

Koplo Diana Angote aliyechunguza kesi ya mauaji ya Asad alimweleza Jaji Lilian Mutende kwamba majirani wa Asad , mtaani Kileleshwa walifichua kwamba “alikuwa akimtusi na kumchapa Maxine.”

Bw Hassan Oyugi aliyetoa ushahidi kortini katika kesi inayomkabili Maxine ya kumuua mumewe Asad Khan aliambia korti, “Desemba 12,2022 nilimsikia Asad akimtusi Maxine –Mbwa wewe toka kwa nyumba yangu.”

Bw Oyugi aliyefika katika makazi ya Asad baada ya kusikia makelele alisema “nilimsikia Asad akimtukana Maxine-Mbwa toka kwa hii nyumba.”

Koplo Angote alisema alipofika katika makazi ya Asad Desemba 12,2022 alimpata Maxine akifungasha virago vyake kuondoka baada ya kuamriwa atoke.

Aliambia mahakama alikagua mfuko wa Maxine na hakupata nguo zake zikiwa na damu licha ya kudaiwa alikuwa amemjeruhi mumewe.

Koplo Angote alisema ndani ya nyumba ya Asad alipata damu jingi sakafuni.

Alieleza mahakama hakumpata Asad kwa vile alikuwa amepelekwa Nairobi Hospital akiwa hali mahututi kwa kuvunja damu.

Koplo huyo alisema Maxine aliwaambia kwamba Asad alikatwa na kioo cha mlango alioutandika teke akimfuata amchape.

Maxine alisema Asad alizua vurugu aliporudi nyumbani amechelewa Desemba 11, 2022.

Alikuwa ameenda kwenye sherehe kujivinjari na marafiki zake.

Dereva wa magari ya Safari Rally Maxine Wahome (kushoto) akiwa kizimbani mahakama kuu ya Milimani. Picha|Richard Munguti

Akiwa kwenye sherehe Asad alimwandikia ujumbe mfupi na kumwambia amunulie pombe kali maarufu kwa jina Jemson.

Maxine alirejea nyumbani usiku wa manane akampata Asad kwa nyumba amelewa chakari.

Mbali na pombe hiyo pia alikuwa amekunywa dawa za kulevya.

Maxine alieleza polisi punde tu alipowasili Asad alizua ukorofi na kuanza kumtandika.

“Maxine alitoroka na kujifungia katika dari. Aliwapigia wazazi wake ambao walimshauri asalie kwenye dari hadi wafike,” Koplo Angote alisema.

Afisa huyo wa polisi alisema walimpata Maxine kwenye dari.

Alisema aliona kioo cha lango la kuelekea kwenye dari kilikuwa kimevunjwa na pia dirisha.

“Asad alitandika mlango teke ufunguke amfikie Maxine achape barabara. Alikatwa kwenye mguu wake na kioo cha mlango. Vipande vya vioo vilikuwa vimetapakaa mle ndani,” alishuhudia Koplo Angote.

Mahakama  ilielezwa kwenye steakesi kulikuwa na damu na pia ndani ya chuma cha mazugumzo.

Asad alijikata mguu na kuumia alipouchapa mlango teke.

Majirani walimpeleka Nairobi Hospital alilkolazwa hali mahututi.

Nduguye Asad, Bw Adil Khan alimhamisha na kumpeleka hospitali ya Avenue alikofia kutokana na maradhi ya Septicimia.

Mahakama iliambiwa Maxine hakuwa mlevi polisi walipofika kwenye makazi hayo.

Jaji Mutende alielezwa kwamba sampuli kutoka kwa mwili wa Asad ,chupa za pombe ya Jemson, dawa za kisukari na dawa za kulevya Ketamine.

Ripoti ya Mkemia wa Serikali Dkt Muendo Muthini aliyewasilisha ripoti ya vipimo vya sampuli hizo alisema alipata chembe za dawa za kulevya zilizomfanya Asadi awewesuke na kupagawa huku akijihisi mwenye kutenda miujiza kama Spiderman.

Mahakama ilielezwa mmoja akichanganya Jemson na dawa hizo za kulevya hujihisi  binadamu spesheli hata anayeweza kuruka juu ya Nyayo House kama ndege.

Koplo Diana Angote mchunguzi wa kesi dhidi ya Maxine Wahome. Photo|Richard Munguti

Hata hivyo wakili Murgor alisema upande wa mashtaka  uliwanyima ripoti hiyo hadi mapema mwaka huu walipoipata.

Jaji Mutende alimkaripia Koplo kwa kucheka akihojiwa hata akaulizwa na jaji “suala nzito kama hili unacheka badala ya kujibu maswali ya wakili kuhusu uwongo kwamba Asad alipigwa ila ni yeye alijiumiza.”

Bw Murgor alieleza mahakama Maxine hana kesi ya kujibu.

Jaji Mutende alielezwa na Bw Murgor “hakuna shahidi alifika kortini kueleza alimwona Maxine akimjeruhi Asad usiku wa Desemba 12,2022.”

Koplo Angote akihojiwa na Bw Murgor alikiri kwamba aliwasilisha taarifa za uwongo kwamba Maxine hana makazi jijini Nairobi na wala hana kazi anayofanya.

Pia alikiri alidanganya mahakama kwamba Maxine hana mahala pa kuishi jijini Nairobi ilhali alipofika katika makazi ya Asad alimpata akiwa na wazazi wake.

“Mbona ulieleza mahakama Maxine hana makazi jijini Nairobi ilhali ulipoenda kumkamata ulimpata akiwa na wazazi wake.Je ulidanganya mahakama,” Bw Murgor alimwuliza Koplo Angote.

“Ndio nilipotosha na kuidanganya mahakama,” Koplo Angote alijibu.

Shahidi huyo alitolewa jasho kwa kumfungulia mashtaka ya mauaji Maxine kabla ya kupokea ripoti ya Mkemia wa Serikali Dkt Muthini.

Kesi inaendelea.