Michezo

Ubashiri wa OPTA wasema Arsenal ina asilimia 76.2, Man United 0.1 pekee kuwa bingwa wa EPL

Na GEOFFREY ANENE November 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

INGAWA Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) haiwezi kuamuliwa mwezi Novemba, yeyote anafikiria kuwa Arsenal haina uwezo wa kutwaa taji lazima awe anatarajia mabadiliko makubwa sana katika fomu ya timu zinazoshiriki.

Wanabunduki wa Arsenal walipepeta majirani zao Tottenham Hotspur 4-1 kupitia mabao ya Eberechi Eze (matatu) na Leandro Trossard katika mechi za wiki ya 12.

Ubashiri mpya wa kompyuta ya Opta umeshuhudia Arsenal wakiimarisha uwezo wao wa kutawala ligi hiyo ya klabu 20 kutoka asilimia 63.6 hadi 76.2.

Hiyo ni baada pia ya Liverpool na City kupoteza michuano yao. City ni wa pili kwa asilimia 14.0 (chini kutoka asilimia 22.9), wakifuatiwa na Chelsea (3.7 kutoka 2.8), Liverpool (2.3 kutoka 7.0), Aston Villa (1.6 kutoka 1.3), Crystal Palace (1.1 kutoka 0.8), Brighton (0.4 kutoka 0.3), Newcastle (0.2 kutoka 0.1) na Bournemouth (0.1 kutoka 0.4), Tottenham (0.1 kutoka 0.2) na Manchester United (0.1 kutoka 0.4).

Liverpool, ambao ni mabingwa watetezi, na City, walipoteza uwezo baada ya kuonja makali ya Nottingham Forest 3-0 na Newcastle United 2-1, mtawalia.

Ushindi huo ulifanya Arsenal kuimarisha mwanya kileleni kutoka pointi nne hadi sita, huku Chelsea ikirukia nafasi ya pili kutoka nambari tatu baada ya kuchabanga Burnley 2-0.

Cha kuvutia ni kwamba Arsenal na Chelsea watavaana katika vita vya mbili za kwanza ugani Stamford Bridge hapo Novemba 30.

Kumekuwa na matukio sita katika historia ya EPL ambapo viongozi wa ligi wamekuwa mbele kwa angalau pointi sita baada ya mechi 12, na kila wakati timu hizo zilifanikiwa kutwaa ubingwa — Manchester United 1993-1994 (pointi tisa), Chelsea 2005-2006 (sita), Chelsea 2014-2015 (sita), Manchester City 2017-2018 (nane), Liverpool 2019-2020 (nane), na Liverpool 2024-2025 (nane).

Hata hivyo, kumekuwa na matukio matano ya timu zilizokuwa chini ya nafasi ya pili ambazo zilikuwa nyuma ya viongozi kwa pointi sita au zaidi baada ya mechi 12, lakini zikafaulu kuruka kileleni na kutawala msimu huo kwa hivyo bado kuna matumaini kwa wanaofukuza Arsenal.

Mara ya mwisho timu kufanya hivyo ilikuwa City msimu wa 2013-2014, wakati kikosi cha Manuel Pellegrini kilikuwa nyuma ya Arsenal kwa pointi sita baada ya michuano 12, lakini baadaye kikatwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili. Wanabunduki wa Arsenal walimaliza msimu huo wakiwa nambari nne, pointi saba nyuma ya City.

Kwa sasa, City ya Pep Guardiola bado wanaonekana wagombea halisi msimu huu. Licha ya kichapo kutoka kwa Newcastle, City bado wanatabiriwa kushinda taji lao la tano ndani ya miaka sita.

Ushindi wa Chelsea dhidi ya Burnley, ukifuatiwa na kipigo cha Liverpool mikononi mwa Nottingham Forest, uliwasaidia vijana wa Enzo Maresca kuongeza pengo kati yao na vijana wa Arne Slot hadi pointi tano.

Chelsea wavuna ushindi mara tatu mfululizo na sasa wanakamata nafasi ya pili kwa alama 23. Blues wako pointi sita nyuma ya Arsenal, lakini wanaweza kupunguza pengo hilo nusu wanapokaribisha wapinzani wao ugani Stamford Bridge.