AI mpya ya Shamiri kuimarisha afya ya akili miongoni mwa vijana
SHIRIKA la Shamiri Institute, limezindua jukwaa jipya la Akili Unde (AI) linalolenga kuongeza upatikanaji wa huduma nafuu za afya ya akili miongoni mwa vijana barani Afrika.
Teknolojia hiyo, inayojulikana kama shamiriAI, ilizinduliwa Alhamisi wiki jana wakati wa Kongamano la Shamiri 2025 jijini Nairobi, na tayari imetajwa kuwa mojawapo ya ubunifu unaolenga kubadilisha mfumo wa huduma za afya ya akili katika jamii.
Ripoti ya Kenya National Adolescent Mental Health Survey (K-NAMHS) inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 44 ya vijana nchini wana matatizo ya afya ya akili.
Hii inatokea wakati ambapo Kenya ina wataalamu wa magonjwa ya akili 500 ambao wanafaa kuwahudumia watu zaidi ya milioni 50.

Kwa mujibu wa mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa Shamiri Institute, Tom Osborn, teknolojia hiyo haikusudiwi kuchukua nafasi ya mtaalamu, bali kuimarisha huduma zilizopo.
“AI inatuwezesha kufunga mapengo ambayo mifumo ya kibinadamu pekee haiwezi. Inafanya huduma kuwa bora, za haraka na zinazoendana na tamaduni zetu,” alisema.
Jukwaa hili linachanganua mazungumzo ya ushauri nasaha kwa wakati halisi na kutoa majibu kwa watumiaji pamoja na wasimamizi wao.
Lengo ni kuhakikisha ubora wa huduma katika shule na jamii.
AI hiyo pia hutumia mbinu maalum ya kubainisha mahitaji ya mwathiriwa hivyo kusaidia kupunguza dalili za msongo na mawazo huku ikipunguza mzigo kwenye mfumo wa afya ya akili nchini.
Sehemu muhimu ya teknolojia hiyo ni uwezo wa kutambua lugha ya Kiingereza, Kiswahili na Sheng, jambo linaloiwezesha kutambua mazungumzo halisi na mitindo ya lugha inayotumiwa na vijana.
“Teknolojia ya AI hutolewa baada ya kufanyiwa majaribio mapana na baadaye hupitia kwa wasimamizi na wataalamu ili kuhakikisha usalama,” alieleza.

Uzinduzi huu umejiri wakati ambapo Shamiri imetoa matokeo ya utafiti mkubwa uliofanywa kati ya 2021 na 2023, ukihusisha wanafunzi 7,865 katika kaunti nne.
Utafiti huo uligundua kuwa asilimia 30 ya vijana walionyesha dalili za msongo wa mawazo.
Balozi wa Ufaransa nchini Kenya na Somalia, Arnaud Suquet, alipongeza ubunifu huo, akisema Kenya imejidhihirisha kama kitovu cha suluhu za kidijitali katika afya.
“Teknolojia na AI zinaweza kutatua changamoto za kimataifa za afya. Shamiri limeonyesha uwezo wa kufikia vijana popote walipo,” alisema.
Kwa sasa, shamiriAI inajaribiwa nchini kabla ya kufanyiwa tathmini ya kina na wataalamu huru.
Baada ya kukamilika, Shamiri inapanga kuiweka wazi (open-source) ili mashirika mengine barani Afrika yaweze kuiboresha au kuitumia.