Makala

Maxine Wahome kujua hatima yake 2026

November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DEREVA wa Safari Rally, Maxine Wahome anayekabiliwa na shtaka la kumuua mpenziwe Asad Khan atajua hatma yake mwaka ujao 2026.

Jaji Lilian Mutende aliyesikiza kesi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili na miezi tisa alisema atahitaji muda kutathmini ushahidi na mawasilisho ya mawakili.

Na wakati huo huo polisi walimrudishia Maxine simu yake iliyotwaliwa Desemba 2022 kufuatia kifo cha Asad.

Koplo Diana Angote alimrejeshea Maxine simu hiyo kufuatia agizo la Jaji Lilian Mutende aliyesikiza kesi ya mauaji aliyoshtakiwa dereva huyo shupavu wa safari rally.

Simu hiyo ilitwaliwa miaka mitatu iliyopita.

Wakili Philip Murgor, Maxine na wakili Steve Kimathi baada ya kusikizwa kwa kesi. Picha|Richard Munguti

Koplo Angote aliamriwa na Jaji Angote amrejeshee Maxine simu yake baada ya kuungama kwamba wamekamilisha kuichunguza.

Simu hiyo ilitwaliwa Desemba 12,2022 kufanyiwa ukaguzi wa kimaabara kubaini watu waliowasiliana na Maxine Desemba 2022 kabla ya ugomvi kuzuka kati yake na Asad mkesha wa Desemba 12,2022.

Mahakama ilielezwa na Koplo Angote kwamba baada ya vurugu kuzuka Maxine alitoroka na kujifungia kwenye dari la makazi yao mtaani Kileleshwa kaunti ya Nairobi.

Kabla ya kujifungia nje Maxine alikuwa amechapwa na Asad alipokuwa akiulizwa sababu ya kurudi nyumbani akiwa amechelewa Desemba 11,2022.

Maxine alikuwa amehudhuria karamu aliyoandaliwa na dada yake.

Alimpelekea ujumbe Asad na kumweleza yuko kwenye karamu.

Wakili Murgor na Maxine Wahome wakiondoka mahakama kuu ya Milimani Novemba 27, 2025. Picha|Richard Munguti

Asad alimweleza amnunulie pombe kali ijulikanayo Jemson akirudi kutoka kwenye karamu.

Aliporejea Asad alipandwa na mori na kuanza kumchapa. Mahakama ilielezwa tayari Asad alikuwa amebugia mfinyo mkali chupa nzima ya Jemson aliouchanganya na dawa za kulevya.

“Maxine alitoroka kipigo na kujifungia nje kwenye dari hadi pale Polisi walipowasili wakiandamana na wazazi wake kumwokoa,” Koplo Angote alimweleza Jaji Mutende anayesikiza kesi ya mauaji aliyomshtaki dereva huyo wa safari rally.

Asad, Jaji Mutende alielezwa na mashahidi alipiga dirisha na mlango teke bila kiatu na kukatwa na vioo.

Jirani mmoja Hassan Oyugi aliyefika kwenye makazi ya Asad alieleza mahakama kwamba marehemu alikuwa akipiga kelele huku akimtusi Maxine.

Akimnukuu Asad, Oyugi alisema,“Nilimsikia Asad akimtusi Maxine-Mbwa hii toka kwa hii nyumba.”

Oyugi alieleza korti Maxine alimjibu kwa sauti hafifu na nyonge na kumweleza “nitatoka.”

Oyugi na majirani wengine waliofika kwa Asad waliambia korti walimpata akivunja damu.

Alipekekwa Nairobi Hospital ambapo iliguduliwa mshipa mkuu unaotwaa damu kutoka kwenye mguu wa kulia hadi moyoni ulikuwa umekatwa na kioo.

Koplo Diana Angote akiwa kizimbani katika kesi ya Maxine Wahome. Picha|Richard Munguti

Asad alidodokwa na damu jingi na cha kuzirai.

Alipelekwa Nairobi Hospital akiwa hali mahututi.

Alihamishwa na kuepelekwa Avenue Hospital Desemba 12,2022 ambapo aliaga baada ya siku sita.

Akiwa amelazwa Asad alipata maradhi ya Septicemia yaliyopelekea kuaga kwake..

Awali Adil Khan, nduguye marehemu alikuwa ameeleza polisi kwamba Maxine ndiye alimjeruhi Asad kabla ya kuaga.

Pia Adil alikuwa ameeleza polisi kulikuwa na watu zaidi ya mmoja ndani ya nyumba ya Asad Kileleshwa waliomshambulia lakini ilibainika baadaye ni yeye (Asad) alijiumiza kwa kutandika dirisha na mlango mateke.

Baada ya ukaguzi kufanyiwa simu ya Maxine na mtaalam wa masuala ya kiteknolojia Timothy Nyende ilibainika mshtakiwa aliwasiliana na marehemu (asad) mara 76,000 kati ya Desemba 11 na 12,2022.

Koplo Angote alimrudishia Maxine simu kufuatia agizo la Jaji Mutende alipoungama hakuna ushahidi waliopata kwenye simu hiyo kuhusu kifo cha Asad.

Ombi Maxine arudishiwe simu iliwasilishwa na wakili Steve Kimathi anayemtetea akiwa na wakili mwenye tajriba ya juu Philip Murgor na Andrew Musangi.

Dereva wa magari ya Safari Rally Maxine Wahome (kushoto) akiwa kizimbani mahakama kuu ya Milimani. Picha|Richard Munguti

Kimathi aliomba Maxine akabidhiwe simu yake kiongozi wa mashtaka Sarah Agweno kufunga kesi dhidi ya Maxine.

Mabw Murgor na Kimathi waliomba mahakama imwachilie huru Maxine kwa vile hakuna ushahidi wowote uliotolewa kumuhusisha na kifo cha Asad.

Jaji Mutende alimwagize Murgor awasilishe tetezi za kuachiliwa kwa Maxine katika muda wa siku 15.

Agweno alipewa siku 15 kujibu.

Kesi hiyo itaamuliwa kati ya Januari na Machi 2026.

Jaji Mutende alisema atatoa arifa katika mtandao wa Idara ya Mahakama siku atakayosoma uamuzi ikiwa Maxine yuko na kesi ya kujibu.

Maxine amekana alimuua Asad. Yuko nje kwa dhamana.