UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vipengele vinavyosawiri jinsi Isimu na Isimujamii zinavyokamilishana
Na MARY WANGARI
LICHA ya kwamba vipo vipengele kadha vinavyofautisha isimu na isimu jamii jinsi tulivyoviainisha, ni dhahiri kuwa taaluma hizi hukamilishana na vilevile hutegemeana, kwa maana kuwa ili kimoja kiwepo lazima kingine kiwepo.
Mkamilishano wa taaluma hizi huweza kuonyeshwa jinsi ifuatavyo;-
Kama anavyosema Mekacha (2000:22), isimujamii inapobainisha uhusiano uliopo wa kijamii kati ya vilugha vilivyomo ndani ya lugha moja hutumia isimu ambayo ndiyo sayansi ya lugha. Hivyo, ili isimujamii ifikie lengo hili hutumia njia ya sayansi ya lugha (isimu). Kwa kufanya hivyo hudhihirisha utegemezi na mkamilishano uliopo baina ya isimu na isimujamii.
Mwanaisimujamii huanza kwa kujiuliza maswali kama vile; Je, kutokana na tofauti za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki inawezekana kubainisha vilugha gani katika lugha moja?
Hivyo basi mwanaisimujamii ili aweze kubainisha vilugha vilivyopo katika lugha moja itambidi aihusishe isimu ambayo ndiyo taaluma ya sayansi ya lugha. Na kwa kufanya hivyo huonyesha mkamilishano.
Aidha, katika kutafiti na kufafanua tofauti tofauti zilizopo ndani ya lugha isimu kama taaluma inayojishughulisha na kufafanua tofauti za lugha kwa njia ya kisayansi ni lazima ishirikiane na isimujamii kama taaluma inachunguza matumizi ya lugha katika jamii. Kutegemeana kwa taaluma hizi mbili husababisha ukamilishano baina ya isimu na isimujamii.
Aidha, isimujamii hutafiti na kufafanua nafasi ya lugha katika jamii kama lengo mojawapo, katika kufanya hivyo hutumia isimu, kwa kuwa isimu ni sayansi ya lugha hivyo ni lazima mbinu za kiisimu zitumike ili kufikia lengo hilo.
Mbinu za kisayansi
Hivyo basi kitendo cha kutumia mbinu za kisayansi katika lengo hili la kuitafiti na kuifafanua nafasi ya lugha katika jamii ndiyo huonyesha ukamilishano huo kati ya isimu na isimujamii.
Mkamilishano mwingine katika ya isimu na isimujamii upo katika isimujamii ya mawandafinyu. Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011:12) wanasema kwamba, mwanaisimu Labov (1972) katika utafiti wake alioufanya katika jiji la New York Marekani kwa lengo la kutaka kujua sababu za tofauti za uzungumzaji, amechunguza na kufafanua maswala ya isimujamii kwa mtazamo wa kiisimu katika kuelezea isimujamii.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]
Marejeo:
Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili ni Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318
Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.
Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili in Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.