Habari za Kitaifa

Mawaziri wa IGAD wakubali kuimarisha ulinzi wa wakimbizi

Na NDUBI MOTURI November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Mawaziri kutoka mataifa saba ya Afrika Mashariki na Ukanda wa Pembe ya Afrika wamefufua upya dhamira yao ya kuimarisha ulinzi kwa wakimbizi na kupanua mbinu za kuwajumuisha mamilioni ya watu wasio na makao katika eneo hilo, kufuatia mazungumzo ya ngazi ya juu mjini Nairobi siku ya Alhamisi.

Chini ya mwavuli wa Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali za Kieneo (IGAD), maafisa kutoka Djibouti, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na Kenya waliidhinisha tamko la pamoja lililosisitiza mifumo kadhaa ya kikanda yenye lengo la kupunguza mzigo kwa nchi zinazowahifadhi wakimbizi na kuboresha hali kwa wakimbizi, waliotimuliwa makwao na wakimbizi wa ndani.

Katibu Mtendaji wa IGAD, Dkt Workneh Gebeyehu, alihudhuria kikao hicho pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia, mashirika ya Umoja wa Mataifa na makundi yanayoongozwa na wakimbizi. Alihimiza serikali kukabiliana na hali ya wakimbizi kwa “uwazi, umoja na dhamira thabiti,” akibainisha kuwa uhamaji si tukio la muda tena bali ni uhalisia unaokumba kanda.

“Katika eneo ambako watu milioni 26.3 wanaishi mbali na makwao si kwa hiari bali kwa mazingira, hatuwezi tena kufikiria uhamaji kama jambo la nadra,” alisema. “Umefumwa katika historia yetu, uchumi wetu na hata jiografia yetu.”

Alionya pia kuwa kiwango cha uhamisho kimevuka rekodi za kihistoria. “Kuna watu milioni 123 wamekosa  makao kote duniani—wa kutosha kuizunguka dunia mara mbili,” Dkt Workneh alisema. “Kama wangekuwa taifa, wangekuwa nchi ya kumi kwa ukubwa duniani, ilhali bila ardhi wala sauti yao wenyewe.”

Kenya, iliyokuwa mwenyeji wa mkutano huo, ilitumia jukwaa hilo kufafanua hatua za karibuni za kuboresha ujumuishaji wa wakimbizi. Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, alionyesha hatua zilizopigwa katika elimu na afya, akisema serikali inalinganisha mageuzi yake na ahadi za kikanda chini ya Tamko la Nairobi na Tamko la Mombasa.

“Zaidi ya wanafunzi 121,000 katika shule zilizoko kambini sasa wananufaika na mlo wa shule, na wanafunzi wa jamii za wakimbizi na wenyeji wanaendelea kupata ufadhili wa Elimu ,” alisema Bw Murkomen, akieleza elimu kuwa nguzo muhimu ya kujitegemea.


Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen (kushoto), akisaini hati ya azimio wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Kanda wa IGAD katika Hoteli ya Safari Park, Nairobi, Novemba 27, 2025, ambapo mawaziri wa kikanda walithibitisha upya ahadi za kuimarisha ulinzi na ujumuishaji wa wakimbizi.
Picha: Wilfred Nyangaresi | Nation

Katika sekta ya afya, alisema Kenya imepanua upatikanaji wa huduma kwa wakimbizi sambamba na Azimio la Mombasa la 2022 kuhusu Afya ya Wakimbizi na Kuvuka Mipaka. “Zaidi ya wakimbizi 100,000 sasa wameandikishwa katika Hazina  ya Afya ya Jamii.”

Alisema hatua hizo zinaonyesha nia ya Kenya kuongoza kwa vitendo wakati eneo hili linapolenga kuoanisha sera za wakimbizi na kuimarisha uratibu wa kuvuka mipaka.

Dkt Workneh alitaja mwamko kama huo katika nchi nyingine za IGAD, akitaja kuimarishwa kwa mifumo ya hifadhi nchini Djibouti; ujumuishaji wa wakimbizi katika mipango ya maendeleo ya kitaifa nchini Ethiopia na Kenya; mfumo wa kujitegemea wa Uganda; juhudi za Somalia za kuwarejesha wananchi; na ushirikiano unaokua wa kuvuka mipaka unaohusisha Sudan Kusini na Sudan.

Hata hivyo, alionya kuwa mishtuko ya hali ya hewa, shinikizo la kiuchumi na mizozo inayoendelea vinaweza kuhatarisha mafanikio hayo. “Bila mifumo imara na iliyoratibiwa, misukumo hii itaongezeka tu,” alisema.

Mkutano wa Nairobi unajengwa juu ya ahadi za kikanda zilioanza na Azimio la Nairobi la 2017, lililoweka mkakati wa suluhisho la kudumu kwa wakimbizi wa Somalia. Makubaliano yaliyofuata huko Djibouti, Kampala na Mombasa yalilenga kupanua wigo ili kujumuisha elimu, ajira, stakabadhi na ushirikiano wa kuvuka mipaka.

Azimio la 2023 kati ya IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki lilisukuma zaidi jitihada za kupata mbinu ya pamoja ya kikanda kukabiliana na uhamisho wa lazima.

Katika ahadi yao mpya, mawaziri walisisitiza pia haja ya kutekeleza kikamilifu mifumo hiyo ya awali, ikiwemo Mfumo wa Sera wa IGAD kuhusu Ulinzi wa Wakimbizi na ahadi zilizotolewa katika Mikutano ya Kimataifa ya Wakimbizi ya 2019 na 2023. Walitaja pia nyaraka za bara na kimataifa kama vile Mkataba wa Wakimbizi wa OAU wa 1969 na Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi kama nguzo za kujenga uimara wa muda mrefu kwa jamii zilizohamishwa.

Mazungumzo ya Nairobi yalivutia ushiriki mpana wa washirika, kutoka UNHCR na UNDP hadi JICA, Cities Alliance na taasisi za utafiti. Jambo la kuvutia zaidi ni kujumuishwa rasmi kwa makundi yanayoongozwa na wakimbizi na asasi za kiraia, hatua inayolenga kuimarisha sera za kikanda kwa uzoefu halisi wa walioathirika.

Nchi saba za IGAD zinahifadhi baadhi ya idadi kubwa na ya muda mrefu zaidi ya wakimbizi duniani, wengi wao wakikimbia machafuko Sudan Kusini, Somalia, Sudan, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo.