Kulikuwa na wizi wa waziwazi, asema Kalonzo akiashiria Upinzani utaenda kortini
KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka amesema kuwa upinzani utaelekea mahakamani kupinga matokeo ya chaguzi ndogo za Mbeere Kaskazini na Malava akidai kulikuwa na wizi wa wazi wa kura.
Bw Musyoka alishutumu serikali kwa kuwasaidia wawaniaji wa UDA kwa kuiba kura kimabavu na kuwazuia wanaotoka ngome zao kupiga kura.
Leo Muthende wa UDA alishinda Mbeere Kaskazini huku David Ndakwa akiwika Malava.
Akizungumza na waumini katika Kanisa la AIC Mukuni, Kaunti ya Machakos, Bw Musyoka alidai kuwa vyombo vya usalama vilitumiwa vibaya kuhakikisha serikali inapata ushindi.
“Wakenya wengi hasa Malava na Mbeere Kaskazini wana hasira. Polisi wakishirikiana na wahuni, waliwatishia wapigakura. Tuna ushahidi ambao tutaupeleka kortini,” akasema Bw Musyoka.
Alidai kuwa Rais William Ruto mwenyewe aliwapigia simu wakuu polisi Mbeere Kaskazini na Malava kuhakikisha wawaniaji wa UDA wanashinda.
“Anajua hakushinda Malava, Mbeere Kaskazini. Tuna ushahidi aliwapigia makamanda wa polisi wahakikishe Bw Muthende anashinda. Dunia nzima inajua ujanja alioutumia kupata ushindi,” akaongeza Bw Musyoka.
Kiongozi huyo pia alikashifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) akisema kulikuwa na ukosefu wa uwiano kwenye takwimu katika baadhi ya vituo vya upigaji kura.
Alisema kuwa kesi yao pia itajumuisha baadhi ya mawaziri walioshiriki kampeni ya kumvumisha Bw Muthende.
Bw Musyoka alikuwa akizungumza wakati wa kusherehekea ushindi wa Antony Kisoi ambaye alichaguliwa diwani wa wadi ya Mumbuni kwa kura 3,849.
Aliwabwaga Harrison Wambua wa Maendeleo Chap Chap na Misi Mutua wa UDA waliozoa kura 2776 na 809 mtawalia.
Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti alisema ushindi huo ulionyesha kuwa Kalonzo bado ni kigogo wa siasa za Ukambani.
Alisema wapigakura waliwasilisha ujumbe kuwa licha ya ziara yake na miradi aliyoanzisha, hawako tayari kumuunga mkono Rais William Ruto mnamo 2027.