Waasi wa ODM na UDA chaguzi ndogo wapangiwa kuadhibiwa
WANASIASA wakuu katika vyama vinavyounda Serikali Jumuishi, waliounga mkono wagombeaji wa vyama vya upinzani katika chaguzi ndogo wiki jana wanakabiliwa na shoka.
Duru zimelezea Taifa Leo kwamba huenda wanasiasa hao wakapokonywa nafasi za uongozi wa kamati bungeni au hata kutimuliwa katika vyama vyao.
Baadhi ya wanasiasa hao, wa chama tawala cha UDA na ODM waliwapigia debe wagombeaji wa Muungano wa Upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Duru zinaongeza kwamba Serikali Jumuishi inalenga kufanya mabadiliko katika uongozi wa kamati mbalimbali bungeni ili kuakisi mpangilio wa sasa wa kisiasa baada ya kukamilika kwa chaguzi ndogo katika maeneo 24 ya uwakilishi.
Serikali jumuishi ilishinda viti vingi licha ya upinzani mkali kutoka kwa Upinzani, ulioungwa mkono na baadhi ya wanachama waasi wa UDA na ODM.
Baadhi ya wanasiasa wanaolengwa kuadhibiwa ni Naibu Gavana wa Homa Bay, Oyugi Magwanga, Kiranja wa Wengi katika Seneti Boni Khalwale, wabunge Mohamed Ali (Nyali), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), Clive Gesairo (Kitutu Masaba), Majimbo Kalasinga (Kabuchai) na Caleb Amisi (Saboti).
Katika kaunti ya Homa Bay, Bw Magwanga alikaidi bosi wake, Gavana Gladys Wanga, kwa kumfanyia kampeni mgombeaji huru Philip Aroko badala ya Boyd Were wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kasipul.
Bw Magwanga alikuwa ameisuta ODM kwa kumpendelea Bw Were wakati wa kura ya mchujo.
Baadhi ya viongozi wa ODM katika kaunti ya Homa Bay, akiwemo Gavana Wanga, tayari wameanzisha shinikizo za kumtaka Bw Magwanga ajiuzulu.
“Mtu hawezi kuhudumia serikali yako na wakati huo kuongea vibaya kuhusu utawala,” Bi Wanga akasema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar amewataka viongozi wa chama hicho, hasa wabunge wajiuzulu. Akiongea Ijumaa, alisema kuwa wanasiasa kama hao wanapaswa kujiunga na vyama walivyoviunga mkono katika chaguzi ndogo wiki jana.
Katika kaunti ya Kakamega, Dkt Khalwale ambaye ni Seneta wa Kaunti hiyo aliunga mkono Seth Panyako wa chama cha DAP-K
aliyeshindani na David Ndakwa wa UDA katika uchaguzi mdogo wa Malava.
Naye Bw Ali alimpigia debe Stanley Kenga wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Magarini, kaunti ya Kilifi.
UDA iliyomdhamini Bw Ali bungeni ilimuunga mkono Harrison Kombe wa ODM aliyeibuka mshindi.
Duru zimeiambia Taifa Leo kwamba UDA sasa inalenga kumpokonya Dkt Khalwale wadhifa kiranja wa wengi katika Seneti huku Bw Ali akipigwa kalamu kama Kamishina wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC).