Timu zilizoonyeshwa kadi nyekundu 17 zarejea uwanjani kwa kishindo
SIKU nne baada ya kupoteza dhidi ya Blooming katika mchezo uliogeuka kuwa sinema ya vurugu iliyoshuhudia kadi nyekundu 17 kutolewa, Real Oruro waliweza kujipangusa vumbi, wakafuta makali ya vitoa machozi, na kurejea kwa kishindo uwanjani Jumamosi, Novemba 29, 2025.
Oruro walichapa Tomayapo 5–2 katika Ligi Kuu ya Bolivia, wakikumbusha ulimwengu kwamba bado wanaweza kufunga mabao bila kutumia ngumi, karate, au kuhitaji polisi kuingilia kati.
Mabao ya Oruro yalifungwa na Luis Vila (mawili), Julio Vila, Alexis Felix Bravo Adan, pamoja na zawadi ya bao la kujifunga kutoka kwa Fernando Aguilar wa Tomayapo.
Tomayapo walikuwa wameongoza mara mbili, kwanza 1-0 kupitia Danny Marcos Perez Valdez na kisha 2-1 kupitia Santiago Cuiza.
Lakini mara tu Josue Castillo alipopata kadi nyekundu dakika ya 50, milango ya mabao ilifunguka, safu ya ulinzi ikapagawa, na ubao wa matokeo ukaanza kung’aa kama mti wa Krismasi.
Oruro wakaongeza mabao manne bila jibu, kana kwamba wanasema, “Tazama, tunaweza kupigana kwa miguu, si kwa makonde.”
Ushindi huo wa kusisimua ulipatikana siku nne tu baada ya mechi ya robo-fainali ya Kombe la Bolivia, mchuano ambao huenda ukawa funzo maalum kwa waamuzi.
Mchezo huo ulitamatika 2–2 huku Blooming ikiponyoka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 na kujikatia tikiti ya kunogesha nusu-fainali.
Lakini hakuna aliyekuwa anazungumzia ufanisi wao kwani gumzo lilielekezwa kwenye kadi nyekundu 17 zilizotolewa wakati na baada ya vurugu kali, kiasi cha kuwafanya mashabiki wa UFC kuangalia kwa heshima.
Kiini cha vurugu
Kwa mujibu wa gazeti la El Potosí, vurugu zilianza wakati nyota wa Real Oruro, Sebastián Zeballos, alipoamua “kuongeza ladha” kwa kuwasukuma wachezaji wa Blooming, na kusababisha mihemko ya hasira kupanda.
Mwenzake, Julio Vila, aliingia uwanjani kama mtu anayefanya majaribio ya ndondi, akirusha makonde yaliyopandisha joto la vurugu hizo hadi kuwa kama mlipuko wa volkano.
Drama haikuishia hapo. Kocha wa Oruro, Marcelo Robledo, alijitosa kwenye mabishano na mmoja wa maafisa wa benchi ya kiufundi ya Blooming na kuishia kuanguka chali, tukio ambalo watu kwenye mitandao ya kijamii waliligeuza meme na kulicheza tena na tena na tena – wengine wakimwonea huruma huku wengine wakitoa kejeli za kuvunja mbavu!
Hali ilipozidi kuwa mbaya polisi wa Bolivia walilazimika kutumia vitoa machozi kutuliza vurugu, wakidhihirisha tena kwamba soka nchini Bolivia haina wakati wa kuchosha.
Ripoti ya mechi baadaye ilithibitisha hesabu hiyo ya kushangaza ya jumla ya kadi 17: nane kwa wachezaji wa Blooming, nne kwa wachezaji wa Oruro, na tano kwa benchi za kiufundi. Usiku wa kihistoria kweli, ingawa si kwa sababu nzuri kama ilivyotazamiwa.
Blooming ilitarajiwa kurejea uwanjani Jumapili, Novemba 30 kwa mpepetano wa ligi dhidi ya wenyeji Oriente Petrolero.
Hata kabla ya joto kutulia Real Oruro na Blooming zitavaana tena kwa mechi ya ligi hapo Desemba 7, 2025.