Habari za Kitaifa

Hafla ya Gachagua ya ibada ya shukrani kanisani ilivyovamiwa na wahuni

Na KEVIN CHERUIYOT December 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IBADA ya kutoa shukrani kwa ushindi wa Diwani mteule wa Kariobangi Kaskazini David Warui Jumapili ilivurugwa baada ya kundi la vijana waliobeba silaha butu kuvamia kanisa ambako maombi hayo yalikuwa yakiendeshwa na kuwajeruhi watu wanne.

Bw Warui, ambaye aliwania kwa tiketi ya chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) aliwashinda wagombeaji wengine tisa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi Novemba 27, 2025.

Ilibidi maafisa wa polisi kuingilia kati fujo hizo zilipotokea nje ya Kanisa la PCEA Berea katika mtaa wa Kariobangi North.

Kisa hicho kilitokea baada ya kukamilika kwa ibada hiyo iliyohudhuriwa na kiongozi wa chama cha DCP, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mashahidi waliambia Taifa Leo kwamba ibada iliendelea vizuri hadi pale waumini walipotoka nje ili wahutubiwe na Bw Gachagua, ndipo fujo zikalipuka.

Kulingana na shahidi mmoja, Peter Kamau, vijana hao waliwasili kwa bodaboda “wakiwa wengi” wakionekana wenye nia ya kuzua vurugu.

“Kila kitu kiliendelea vizuri. Tulikuwa nje ya kanisa tukimsubiri Gachagua aongee. Ghalfa, wahuni walifika kwa pikipiki wakirusha chupa na kuwashambulia watu,” akasema.

Watu hao wanne walijeruhiwa wakati ambapo umati wa watu ulitawanyika, huku wengine wakijaribu kujikinga.

“Wahuni hao walikuwa wamebeba visu na silaha zingine butu. Walianza kushambulia kanisa kwa mawe na kuharibu magari,” Bw Kamau akaongeza.

Maafisa wa polisi walijibu kwa kuwarusha vitoza machozi na kufyatua angani risasi za chuma ili kuwatawanya wavamizi hao.

Moshi wa vitoza machozi ulienea hadi ndani ya kanisa, na kulazimisha waumini kujikinga.

“Hiki ni kitendo kibaya zaidi. Humu mna watoto na wakongwe. Mbona watufanyia hivi?” akauliza Bi Grace, mmoja wa wanachama wa kanisa hilo huku akilaani shambulio hilo.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni Simon Thuku, aliyedungwa kisu kwenye bega la kulia alipokuwa akimsaidia binamu yake alijeruhiwa mguuni.

Binamu huyo pia aliripoti kupoteza simu yake na pesa wakati wa fujo hizo.

Usimamizi wa Hospitali ya Mama Margaret Uhuru ulithibitisha kuwapokea watu wanne waliojeruhiwa.

Mmoja wao, baadaye alisafirishwa hadi Hospitali ya Mama Lucy Kibaki kwa matibabu maalum.

Utulivu uliporejea, Bw Gachagua alitumia fursa hiyo kutoa kudokeza mpango wa Umoja wa Upinzani katika kaunti ya Nairobi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Alidokeza kuwa huenda kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akateuliwa kuwa mgombea urais wa Umoja wa Upinzani.

Aliongeza kuwa yeye na Bw Musyoka wamekubaliana kuhusu mkakati wa ugavi wa viti vikuu vya kisiasa katika kaunti ya Nairobi kuelekea 2027.

“Tumekubaliana kwamba gavana, seneta na mwakilishi wa kike atatoka chama cha DCP. Aidha, vyama vya Wiper na DCP vimeazimia kushinda jumla ya viti 16 kati ya 17 vya ubunge katika kaunti ya Nairobi na viti 73 kati ya 85 vya udiwani,” akaeleza.

Bw Gachagua pia alijitenga na kuangushwa kwa upinzani katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ambapo Leonard Wa Muthende wa UDA alimshinda Newton Kariuki wa chama cha DP kwa kura 494 pekee.

“Sikudhamini mgombeaji huko. Nilienda tu kusaidia wenzangu wa upinzani. Mgombeaji wao alishinda lakini ushindi wake ukatwaliwa na serikali,” akadai, akisisitiza kuwa hawajibiki kwa njia yoyote na matokeo hayo.

Bw Gachagua alisema kuwa chama chake cha DCP kilishiriki katika chaguzi ndogo katika wadi tano na kikashinda tatu na kuibuka nambari mbili katika chaguzi mbili.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA