SI kawaida kupata wanawake Wakenya wakifanya kazi ya kuchomelea vyuma. Hata hivyo, haimaanishi hawapo kama wanawake hawa wawili ambao Taifa Leo Dijitaliilipata katika eneo la viwandani la Kariobangi Light Industries wakichapa kazi inayodhaniwa na wengi kuwa ya wanaume tu.
Wanawake hao Julia Wamboi na Kellen Wanjiku walionyesha ujuzi wa hali ya juu na ari ya kuchapa kazi hiyo jinsi wanavyofanya wanaume.
Mwandishi huyu alizuru karakana ya Mukish Electrical Engineering Works na kuwapata wamezamia shughuli ya kuunda maboksi ya mita za stima yanayowekwa ukutani katika majengo ya biashara, taasisi mbalimbali za elimu, hospitali, makazi na kadhalika.
Walielezea mwandishi huyu hadithi yao ya kusisimua jinsi walivyoanza kazi hii ambayo sasa wanasema wanaipenda sana.
Karakana hii inapatikana karibu na makutano ya barabara ya Outering Road na Komarock Road mtaani Kariobangi jijini Nairobi.
Wamboi, ambaye ana umri wa miaka 37, amefanya kazi hii miezi sita. Anasema alipatwa na mshangao alipoingilia kazi hii akiulizwa kutumia chombo ambacho hakuwa amewahi kukitumia maishani mwake.
“Mimi sijafanya hii kazi kwa muda mrefu. Kilichonileta hapa ni hali ngumu ya maisha. Nilitaka kujitafutia riziki. Niliwasili hapa nikiwa sijui kukata chuma ama kutumia vyombo vinavyopatikana katika karakana kama ‘grinder’, ‘drill’, msumeno na vinginevyo. Sikuwa na ujuzi wowote wa kazi hii ya kuchomelea.
“Hata hivyo, sikuiona ikiwa kazi ngumu kwa sababu nilijitolea kwa moyo wangu na kuwekeza muda wangu mwingi kuifahamu.
“Siku zangu za kwanza katika kazi hii nilikuwa nasalia na mshangao nilipoambiwa hebu fanya hiki ama kile ukitimia ‘grinder’ na vyombo vinginevyo kwa sababu sikuwa nimewahi kuvitumia. Hata hivyo, nilisaidiwa sana na wafanyakazi wenzangu kufahamu kazi hii na naifanya vyema.
“Sikuenda chuo chochote cha mafunzo ya uchomeleaji wa vyuma; nilijifunza hapa tu. Nakumbuka nilipoomba kazi hapa, niliulizwa, je, utaiweza? Nilijibu ndio nitaweza na hivyo ndivyo niliipata.
“Watoto wangu hawana tatizo na kazi nyangu. Hata ndugu zangu wamekuwa wakinipa moyo wakisema niifahamu vyema kabisa halafu nijiendeleze katika uwekaji wa waya za stima, yaani niichukulie kama kozi.
“Wakati huu ninafahamu vizuri kazi hii na kutumia vyombo mbalimbali vinavyopatikana hapa. Hapa, tunaunda maboksi ya kuweka mita za stima pekee.
“Sisi hufika kazini saa mbili asubuhi kila siku kutoka Jumatatu hadi Jumamosi na kufunga siku saa kumi na mbili jioni. Tunapumzika Jumapili pekee yake. Wanawake hawafai kukaa nyumbani tu ama kuuza miili yao kupata riziki yao. Hakuna kazi ambayo mwanamke hawezi kufanya. Sisi hapa tuko tayari kufunza mwanamke yeyote ambaye angependa kazi ya kuchomelea vyuma. Tutamsaidia jinsi nilivyosaidiwa.”
Kellen Wanjiku, 37, ambaye ni mama wa watoto watatu, ndiye alivutia Wamboi kiasi cha kuwa mchomeleaji. Alituonyesha jinsi ya kuunganisha vyuma, sehemu muhimu katika kazi hii ya uchomeleaji. Safari ya Wanjiku katika kazi hii ilianza miaka miwili na nusu iliyopita. Kama Wamboi, aliwasili katika karakana hii bila ujuzi wowote wa kuchomelea. “Lazima uwe na hamu kubwa ya kufahamu kazi hii ndiposa ufaulu. Inategemea pia kiwango cha kuhusika kwako katika kuifahamu. Ilinichukua miezi sita kufahamu vyombo hivi na jinsi ya kuvitumia. Na niliipenda.”
Wanjiku, ambaye alikuwa muuzaji wa matunda na mboga kabla ya kibanda chake kubomolewa, anasema kwamba soko la maboksi ya mita za stima wanayotengeneza ni viwanda pamoja na kampuni ya kusambaza umeme ya Kenya Power na watu binafsi. “Ukubwa wa maboksi tunayounda ni kutoka 14 hadi 18. Nimekuwa nikifanya kazi hii kwa miaka miwili na nusu. Tunakamilisha maboksi matano kila siku.”
Mchomeleaji huyu wa vyuma anasema kwao utepe ni kama kitabu na ‘scriber’, ambayo ni waya inayotumiwa kuchora laini kwenye vyuma, ni kalamu yao. “Lazima uwe na vitu hivi pamoja na msasa na tupa ndogo katika koti lako la kazi.”
Kevin, ambaye ni mmoja wa wanaume saba wanaofanya kazi ya kuchomelea, amesifu sana wanawake hao wawili. “Kazi hii haihitaji mtu anayeogopa kufanya makosa. Ukifanya makosa halafu useme, unapata kurekebishwa. Tofauti na baadhi ya wanaume ambao wako hapa wanaogopa kukosea na hivyo kupoteza katika kufahamu kazi hii vyema, wanawake hawa wamekubali kazi hii. Walifanya makosa wakianza, lakini walikubali kurekebishwa na sasa ni wachomeleaji vyuma stadi,” alisema Kevin, ambaye amefanya kazi hii kwa miaka mitatu.
Wamboi na Wanjiku walikiri mambo si rahisi katika karakana. Walielezea baadhi ya changamoto wanazopitia. “Ukiangalia mikono yetu ina alama ya kukatwa na chuma ama msumeno. Lazima uwe muangalifu sana katika kazi hii la sivyo utajipata na majeraha mengi,” wanasema, huku Wanjiku akionyesha mwandishi huyu alama moja aliyopata kutokana na ‘grinder’ kumkata juu ya mguu. “Vyuma pia vinaweza kukuingia machoni unapochomelea bila helmeti. Kuna kemikali tunayotumia kulainisha maboksi kabla yapakwe rangi ambayo pia huwasha ngozi. Tunatumia msasa kwanza kabla ya kulainisha na kemikali hiyo.”
Mshahara
Licha ya biashara hii kuwa na soko kubwa linaloletea mmiliki mamilioni ya fedha za Kenya kila juma, wafanyakazi katika karakana hii walikiri kwamba hawapati mishahara ya kuridhisha. “Malipo si mazuri sana, lakini sina kazi mbadala,” alisema Wamboi, huku Wanjiku akifichua kwamba wao hupokea Sh300 kila siku. “Fedha hizi ni ndogo kwa hivyo tunalazimika kupuuza vitu vingine kama kununua viatu spesheli vya kutumia kwenye karakana ya vyuma, ambavyo bei yake ni Sh2,000 kwa jozi moja.”
Kevin, ambaye ndiye mmoja wa wachomeleaji stadi katika karakana hiyo, aliungama kuwa malipo ni ya chini.
Hata hivyo, alifichua, “Kuna waajiri wengi ambao hawawezi kukupa kitu unapoanza kazi kama mwanafunzi. Hapa ni tofauti, unapata kitu, ingawa ni kidogo wakati unajifunza. Kufahamu kazi hii itakuchukua kati ya miezi mitatu na sita. Ukishaifahamu, utaweza kuongezwa mshahara wako, ingawa bado mzuri sana; ule unaokuwezesha kujikimu kimaisha.”
Historia fupi ya wanawake kuchomelea vyuma
Historia inasema wanawake walijitosa katika kazi ya kuchomelea wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 na 1945. Kujitosa kwao katika kazi hii ni kulitokana na kazi kuwa nyingi sana kwa wanaume.
Nayo tovuti moja nchini Marekani iliripoti mwaka 2015 kwamba kuna asilimia tano pekee ya wachomeleaji vyuma wanawake nchini humo. Wizara ya Leba ya Marekani ilitabiri idadi yake ya wachomeleaji itafikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2020.
Kenya ina zaidi ya taasisi 30 zinazofundisha kazi ya kuchomelea vyuma, ingawa ni vigumu kupata takwimu zinazoonyesha wanawake wangapi wanafanya kazi hii.