Habari

UDA yamvua Khalwale wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Seneti

Na CHARLES WASONGA, MARY WANGARI December 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SENETA wa Kakamega Boni Khalwale amevuliwa rasmi wadhifa wake kama Kiranja wa mrengo wa Walio Wengi katika Seneti.

Nafasi hiyo sasa imetunukiwa Seneta wa Bungoma David Wakoli Wafula wa chama cha Ford Kenya, mojawapo ya vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza.

Spika wa Bunge hilo Amason Kingi, Jumanne, Desemba 2, 2025  alithibitisha kupokea waraka kutoka mrengo tawala wa Kenya Kwanza kuhusu mabadiliko.

“Barua hiyo imeandamanishwa na kumbukumbu kuhusu uamuzi uliopitishwa kumwondoa Kiranja wa Wengi Boni Khalwale. Seneta wa Bungoma David Wafula Wakoli ameteuliwa kushikilia nafasi hiyo,” Bw Kingi akasema.

Dkt Khalwale, aliyechaguliwa kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ni miongoni mwa viongozi waliokaidi msimamo wa chama hicho na kuwaunga mkono wagombeaji wa vyama pinzani katika chaguzi ndogo zilizofanyika Novemba 27, 2025.

Seneta huyo wa Kakamega alikuwa mstari wa mbele kumpigia debe mgombea wa DAP- Kenya Seth Panyako katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malava.