Mwalimu mkuu akwamilia kazi ya uvuvi inayochukuliwa ya watu wa tabaka la chini
KATIKA jamii, wengi mara nyingi huuchukulia uvuvi kuwa shughuli inayotekelezwa na watu wa tabaka la chini kwa lengo la kujitafutia riziki.
Lakini kwa Bw Mwenye Hussein Ahmed, 47, hilo ni tofauti kabisa. Bw Hussein ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi na Sekondari Msingi ya Wiyoni iliyoko kisiwani Lamu.
Licha ya kuwa mwalimu mkuu ambaye ana majukumu mazito ya kuongoza shule yake iliyo na jumla ya wanafunzi 611, Bw Hussein amekataa kabisa kuiacha kazi hiyo ya uvuvi, shughuli ambayo amekuwa akiitekeleza tangu utotoni mwake.
Alianza kufanya kazi ya uvuvi akiwa na umri wa miaka 14 pekee na sasa amedumu kwenye sekta hiyo kwa karibu miaka 33.
Kabla ya kujiunga na shule ya msingi, sekondari na chuo cha mafunzo ya walimu kusomea taaluma aliyo nayo sasa, Bw Hussein tayari alikuwa amejizolea tajriba tele katika shughuli za uvuvi ndani na nje ya kijiji chake cha Mtangawanda, kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki.
Anasema uvuvi ulimwezesha kukimu mahitaji yake madogomadogo, akiwa mwanafunzi shuleni na chuoni.
Mara nyingine shughuli hiyo ya uvuvi aliyokuwa akiitekeleza nyakati za wikendi au likizo ndefu ilimsaidia hata kulipa karo. Leo hii akiwa mwalimu, Bw Hussein anasema katu hawezi kuitupilia mbali kazi hiyo.
Yeye ni mwalimu mchana ilhali usiku, wikendi au msimu wa likizo kama wa sasa, hugeukia uvuvi kindakindaki baharini.
Ni shughuli ambayo hakuisomea bali aliweza kuifahamu vyema kupitia kuandamana na marafiki zake, ikiwemo wazee wenye tajiriba kwenye sekta hiyo.
Alipowatazama marafiki zake wakitekeleza uvuvi, Bw Hussein anasema ndivyo na yeye aliigiza, hivyo kuimarika kuwa hodari na mvuvi wa kutegemewa.

Anashikilia kuwa hawezi kuuacha uvuvi kwani ni mojawapo ya mambo anayoyatekeleza na kumpa furaha maishani.
Anasema pia anauchukulia uvuvi kama mbinu mojawapo ya kuupa mwili au misuli mazoezi.
“Licha ya kuwa mwalimu na hata kupandishwa cheo cha kuwa hedimasta, bado sina lengo la kuacha uvuvi. Nauchukulia uvuvi kama sehemu ya maisha yangu. Umenitoa mbali. Baba mzazi alikuwa mkulima ila sikufuata nyayo zake. Nafsi na moyo wangu, vyote viliishia kupenda sana kuvua samaki baharini. Hadi sasa navua,” akasema Bw Hussein.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu (TTC) cha Asumbi kilichoko Kaunti ya Homa Bay mnamo 2002, serikali kuu ilimwajiri moja kwa moja.
Anasema kwa sasa amefundisha kwa miaka 23 lakini bado kila akipata muda yeye huzamia shughuli za baharini.
“Kule baharini hufanya watu kupanuka akili hata zaidi. Wikendi, nyakati za likizo au hata usiku, mimi huingia baharini kuvua ili kujipatia kitoweo, kuuza au hata kutumia pato langu la samaki kusaidia wengine wenye uhitaji katika jamii,” akasema Bw Hussein.
Mbali na kutekeleza uvuvi, Bw Hussein pia amekuwa akiwafunza vijana ambao azma yao ni uvuvi.
Miongoni mwa wanagenzi wake ni mtoto wake Ahmed Mwenye Hussein, 20.
Bw Mwenye ni mtoto wa tatu wa Bw Hussein ambaye ni baba wa watoto wanne.
“Kwa sababu mtoto wangu anapenda shughuli za baharini, nimekuwa nikimfunza kuvua na kwa sasa yeye ni mvuvi shupavu. Kuna wengine wengi ambao ni stadi wa uvuvi baada ya kupitia mikononi mwangu,” akasema Bw Hussein.
Kwa upande wake, Bw Mwenye alimsifu babake kuwa mtu mpole, mwenye bidii na ambaye hapendi kujitukuza.
“Kwanza huwezi kujua kama yeye ni mwalimu, hasa akiwa na cheo cha hedimasta. Babangu anapokuwa baharini, huingiliana na watu wote. Hata anapopita mitaani huwezi kujua ni mwalimu mkuu wa shule. Amenifunza kujishusha na kufanya bidii maishani,” akasema Bw Mwenye.
Mkurugenzi wa Elimu wa Lamu ya Kati, Bi Rukia Ali Abdalla, alimsifu Bw Hussein kwa weledi wake wa kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja.
Bi Abdalla aliwashauri walimu na wafanyakazi wengine wa umma kuiga mienendo yake.
“Yeye ni mwalimu na mvuvi. Hutampata hata siku moja eti taaluma yake ya ualimu imeathiriwa na shughuli zake za uvuvi. Yaani anajua kuendesha mambo kwa wakati mmoja. Hata akistaafu, hatapata shida kwani tayari amekita mizizi katika uvuvi. Ni mfano wa kuigwa,” akasema Bi Abdalla.
Katika shindano la mwaka huu la uvuvi ili kuadhimisha Tamasha ya Utamaduni wa Lamu, Bw Hussein na timu yake walishinda kwani mashua yao ndiyo iliyovua samaki mkubwa na mwenye uzani mzito zaidi.
Samaki huyo aina ya jodari alikuwa na kilo 90.