Shangazi Akujibu

Mama na bintiye wameniteka kimapenzi! Nipe ushauri

December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Shikamoo shangazi. Nimenaswa kimapenzi na msichana fulani. Juzi nilimtembelea kwao kwa mara ya kwanza. Mama yake hajaolewa tena ni mchanga na mrembo sana. Nimechanganyikiwa! Nishauri tafadhali.

Ni wazi kwamba mama ya msichana huyo pia amenasa moyo wako kimapenzi. Sasa unashindwa utamchagua yeye ama ni binti yake. Jipe muda ufikirie kisha uamue. Ninaamini mama amekuzidi umri ingawa hiyo si hoja bora mapenzi.

Nampenda tusiyeonana

Nilijuana na mwanamume fulani kupitia kwa mtandoa na hatimaye tukapendana ingawa hatujawahi kuonana. Huu sasa ni mwezi wa sita tangu tulipojuana. Haya ni mapenzi ya kweli?

Kuna visa kadhaa vya watu waliojuana na kupendana kupitia kwa mtandao na hatimaye wakaoana. Hata hivyo, hatimaye mtahitaji kukutana na kuwa pamoja kwa muda ndipo mjue ukweli wa mapenzi yenu.

Eti ataacha tu mubaba iwapo nitaamua kumuoa

Za kwako shangazi. Kuna mwanamke ninayemtaka lakini amekuwa akinizungusha tu. Hatimaye juzi alifungua moyo wake. Akaniambia ana uhusiano na mtu aliye na familia na atamuacha tu kama niko tayari kumuoa. Nishauri.

Mwanamke huyo amekwambia anachotaka; mume wake mwenyewe. Na ndiyo sababu anataka kwanza umhakikishie kwamba nia yako kwake ni ndoa. Kama unaamini anatosha na uko tayari kwa ndoa, kazi kwako.

Niko shule ya upili ila nimemfia jamaa fulani

Shikamoo shangazi. Nina miaka 16 na ninasoma katika shule ya upili. Kuna mwanamume anayenitaka kimapenzi. Nampenda lakini nahofia mapenzi yataathiri vibaya masomo yangu. Nishauri.

Msimamo wako hasa ndio ushauri wangu kwako. Wewe bado ni mwanamke mchanga na masomo ndiyo tegemeo lako maishani. Mwelezee msimamo wako huo. Kama kweli anakupenda atangojea.