Habari

Kikundi cha kusakata densi chadai umiliki wa ardhi ambayo shule imejengwa

Na NDUBI MOTURI December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MZOZO wa ardhi umeibuka Kamukunji kati ya wanawake wazee wanachama wa kikundi cha utamaduni na shule ya upili ya umma iliyodumu kwenye ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 40.

Kikundi cha Galole Women Dancers, ambacho kina asili yake kutoka kundi maarufu la Nyakinyua, kinasisitiza kuwa ndicho mmiliki halali wa kipande cha ardhi ndani ya ekari saba zinazomilikiwa na shule ya upili ya wasichana ya Maina Wanjigi jijini Nairobi.

Madai yao yamekitwa katika barua ya kutengewa ardhi hiyo na hati ya umiliki kilichopatiwa baada ya upimaji ardhi uliofanywa miaka iliyopita.

Akitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Mipango ya Bunge la Kaunti ya Nairobi, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Halima Gole, alieleza jinsi watu walaghai wanajaribu kunyakua ardhi hiyo.

Anasema ardhi hiyo ilitolewa kwa wanadensi hao na Rais wa Kwanza Mzee Jomo Kenyatta mwaka 1966. Na ni kwenye ardhi hiyo hiyo ambapo aliyekuwa Mbunge wa Kamukunji, Maina Wanjigi, alianzisha ujenzi wa shule hiyo mwaka 1982, mradi uliogharimiwa na wanawake hao kwa ushirikiano na serikali.

Lakini leo, Bi Gole aliambia madiwani kuwa wanawake hao wengi wao wakiwa wazee, wagonjwa na wajane, wanapambana na watu “wasiojulikana” wanaojifanya wawakilishi wa shule ili kuwatimua.

“Wanakuja usiku wa manane, wanavunja nyumba zetu na kutuamuru tuondoke. Nyumba zetu zimeshateketezwa moto mara tatu. Baadhi ya wanachama wetu ni wagonjwa; wengine wamefariki katikati ya sakata hili. Tunataka haki tu. Ardhi hii ni yetu, na tuna stakabadhi kuthibitisha,” aliambia kamati hiyo inayoongozwa na diwani wa Kitisuru, Alvin Palapala.

Ardhi inayozozaniwa ni ya thamani ya takriban Sh210 milioni.

Mzozo huo uliripotiwa rasmi kwa Wizara ya Ardhi na Naibu Kamishna ( DCC) wa Kaunti Ndogo ya Kamukunji, Frederick Martin Muli, ambaye mnamo Machi 13 aliomba Mkurugenzi wa Upimaji ardhi kutuma maafisa katika eneo husika.

Baada ya ukaguzi, Bw Muli alisema hakuweza kubaini iwapo kipande kinachodaiwa na wanawake hao ni tofauti au ni sehemu ya eneo la shule.

Lakini ukaguzi ulisitishwa baada ya mwanamume aitwaye Kariuki kujitokeza, na kumlazimisha DCC kusimamisha mchakato huo.

“Jambo hili linazidi kuwa gumu na lenye utata,” alisema Muli, akibainisha kuwa ardhi ya shule hiyo iliyozungushwa ukuta na Wizara ya Elimu mwaka 2018 bado haina hati ya umiliki, pengo ambalo limefungua mlango kwa watu tofauti kuidai.

Mbunge wa eneo hilo, Yusuf Hassan, na Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Ndogo, Luley Abdullahi Yahya, wanasema ardhi hiyo ni ya shule bila shaka yoyote.

Wanasema madai ya kikundi hicho cha wanawake ni sehemu ya mpango mpana wa kunyakua mali ya umma.

“Kumekuwa na majaribio mengi kunyakua ardhi hii kwa kutumia makundi tofauti,” Bw Hassan alisema awali. “Tunasimama kidete na Shule ya Sekondari ya Maina Wanjigi dhidi ya magenge ya wanyakuzi wa ardhi.”