Verstappen miongoni mwa madereva 68 wa East African Safari Classic Rally Kwale Ijumaa
ALIYEWAHI kuwa dereva wa mbio za magari ya langalanga ya Formula One, Jos Verstappen, atakuwa mmoja wa vivutio kwenye makala ya 11 ya mbio za magari za East African Safari Classic Rally zitakazoanza mjini Kwale hapo Ijumaa, Desemba 3, 2025.
Akishiriki East Africa Safari Classic kwa mara ya kwanza kabisa, baba huyo wa bingwa wa dunia wa Formula One, Max Verstappen, ataendesha gari la aina ya Porsche 911.
East Africa Safari Classic itaanza kwa nguvu kupitia sehemu ya kwanza yenye umbali wa kilomita 376 ikipitia Voi na Milima ya Taita. Kilomita 175 kati ya 376km zitakuwa za mashindano ambayo ni ndefu kuliko baadhi ya matukio ya siku tatu ya Mbio za Magari za Dunia (WRC).
Magari yanayoshiriki ni yale yalijengwa kabla ya Desemba 31, 1985, hatua inayolinda hadhi ya mashindano hayo kama jaribio kuu la uimara wa magari ya zamani.
Kabla ya kuanza kwa mashindano, Wizara ya Michezo iliingilia kati kutatua mgogoro kati ya mashirikisho ya Kenya Motor Sports Federation (KMSF) na Motorsports Kenya.
Waandalizi waliagizwa kuwaruhusu madereva wenye leseni za KMSF kushiriki, hatua iliyorejesha usawa na kuhakikisha ushiriki wa madereva wa ndani, huku suala hilo likisubiri kuamuliwa mahakamani.
Mbio za mwaka huu zimevutia washiriki 68, zikichanganya mabingwa wa mashindano ya umbali mrefu na madereva mahiri kutoka teknolojia za kisasa.
Miongoni mwao ni dereva Jourdan Serderidis kutoka Ugiriki anayefahamika kwenye WRC Safari Rally kutokana na matokeo mazuri ya hivi majuzi ya kuingia 10 bora. Serderidis ameweka kando Ford Puma R1 ya kisasa na kuchukua Porsche 911 iliyotayarishwa na Tuthill kujaribu mtindo wa kizamani wa Classic Rally.
Mabingwa watetezi Eugenio Amos na Paolo Ceci wanarejea wakiendesha Ferrari, lakini wanakabiliwa na sintofahamu kutokana na maandalizi hafifu na mashaka kuhusu uimara wa gari lao.
Amos alisema hali yao ni ya kipekee. “Tuko katika nafasi ya ajabu kwa kuwa sisi ni mabingwa watetezi, lakini hatuna mashine ya kutuwezesha kufanya kama mabingwa,” akasema. Lengo lao la kwanza ni kufika siku ya mapumziko salama, na lengo la muda mrefu ni kumaliza siku zote tisa za mashindano.
Upande wa Kenya unaongozwa na bingwa wa zamani Baldev Chager anayeendesha Porsche 911, mmoja wa wawakilishi bora wa nchi katika harakati za kutafuta ushindi wa jumla.
Pia, yupo mkongwe Glen Edmunds aliyerejea na mwelekezi mpya Joe Autera katika gari la Datsun Violet GT lililotayarishwa na Triple S Motors. Edmunds alionyesha matumaini baada ya kufanya majaribio makali. “Tumekuwa na changamoto kadhaa, lakini ndiyo maana kuna majaribio. Inaonekana tumeyatatua mengi,” akasema, akitumaini kuepuka matatizo yaliyomsumbua mwaka 2023 akipaisha Skoda.
Zaidi ya mashindano, Classic Rally inaendelea kupanua mchango wake katika utalii na maendeleo ya michezo ya magari ukanda huu. Mwenyekiti wa Mashindano, Joey Ghose, alitangaza vitengo viwili vipya vitakavyoanza mwaka ujao: East African Classic Raid na East African Classic Tour.
Classic Raid litakuwa shindano la siku nne lenye umbali wa takriban kilomita 4,000, lililobuniwa kwa washiriki wanaotaka changamoto kali ya kasi na uvumilivu.
Classic Tour, kwa upande mwingine, halitakuwa la ushindani na limekusudiwa kwa wapenda magari wanaotaka kufurahia mandhari nzuri ya Kenya bila shinikizo la muda. Ghose alisema Tour itaimarisha utalii, huku ikiwaruhusu wamiliki wa magari ya zamani kufurahia safari tulivu na ya kipekee nchini.
Imetafsiriwa na Geoffrey Anene