Wataalamu waonya kuhusu uvuvi haramu unaoendelezwa Bahari Hindi
WATAALAMU wa samaki wametoa onyo kuhusiana na kuongezeka kwa uvuvi haramu, usioorodheshwa na usiodhibitiwa (IUU) katika Bahari ya Hindi, kutokana na ukosefu wa uangalizi wa kutosha.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamoja ya Afrika Kuhusu Rasilmali za Wanyama (AU-IBAR), Huyam Salih, alisema kwamba kulinda mito, mabwawa, eneo la majani ya maji, na mifumo ya baharini si tu suala la mazingira bali la lazima kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu.
“Uvuvi wa kupita kiasi na matumizi ya mbinu haramu za uvuvi ndio wasiwasi mkubwa zaidi, lakini ukosefu wa uwezo katika nchi mbalimbali umekuwa kikwazo katika kupambana na vitendo vibaya katika bahari,” alisema.
Dkt Salih alisema uvuvi haramu unatokana na udhaifu wa mifumo ya ufuatiliaji, udhibiti na ukaguzi (MCS) pamoja na mapengo ya utawala, ambayo yanapatikana katika pwani za nchi nyingi zinazoendelea kutokana na ukosefu wa rasilmali na uwezo.
“Bila ufuatiliaji madhubuti, ni vigumu sana kubaini meli, kubaini hali ya idhini yake, na kutekeleza kanuni. Hii inamaanisha meli haramu za uvuvi zinaweza kufanya shughuli zao bila uwezekano wa kukamatwa au kutozwa adhabu,” alisema mkurugenzi huyo wa AU-IBAR.
Mkurugenzi wa Uvuvi na Maendeleo ya Ufugaji Samaki Kenya, Mahongah Joseph, alisema kuwa kuongezeka kwa uvuvi haramu, uchafuzi wa plastiki, na mabadiliko ya tabianchi vimekuwa vikwazo vikuu katika maendeleo ya uchumi wa bahari, si tu Kenya bali barani Afrika.
Akizungumza katika mkutano wa Nne wa Kamati ya Kiufundi wa Mradi uliofanyika Mombasa na kuandaliwa na AU-IBAR, Bw Joseph alisema serikali imekamilisha mkakati wa uchumi wa bahari, ambao utazinduliwa kushughulikia uvuvi kupita kiasi, uchafuzi wa Bahari ya Hindi, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunamalizia sehemu ya uhariri wa mkakati huu, na itasaidia kushughulikia changamoto zinazoongezeka katika bahari pamoja na masuala yanayowakumba wanawake na vijana ambao wanachukua nafasi muhimu katika miradi mbalimbali ya uchumi wa bahari,” alisema Bw Joseph.