Habari

Dhahabu ya damu: Vita vyachacha Kakamega wakazi wakipinga uchimbaji wa dhahabu

Na BENSON MATHEKA December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

DESEMBA 4,2025, iligeuka kuwa msiba kwa familia ya Conrad Ashioya Isese, mfanyakazi wa ujenzi kutoka kijiji cha Imabwa, Ikolomani, Kaunti ya Kakamega, aliyepigwa risasi na kuuawa wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wakipinga mpango wa kuruhusu kampuni ya kigeni kuchimba dhahabu katika eneo hilo.

Ashioya, ambaye alikuwa ameandamana na mfanyakazi mwenzake, Edgar Wekesa, aliondoka nyumbani alfajiri kufanya kazi karibu na soko la Isulu. Alitumwa kuchukua kipimo, milio ya risasi iliposikika, na moja ya risasi ikampata alipokuwa akikimbia katika mtafaruku huo.

“Niliendelea kumpigia simu mara kadhaa, hadi ikajibiwa na mhudumu wa mochari akiniambia mwili wa Ashioya ulipelekwa mochari ya hospitali ya rufaa ya Kakamega,” alisema Wekesa.

Ashioya alikuwa miongoni mwa watu wanne waliouawa wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji wakiwemo wachimbaji wadogo wa dhahabu waliokuwa wakipinga kikao cha ushirikishaji wa umma kilichoandaliwa na Nema na Kampuni ya Shanta Gold kuhusu kuwhamishwa kwa familia 800 kufuatia kugunduliwa kwa madini hayo yenye thamani ya Sh683 bilioni.

Zaidi ya kilomita 48 kutoka Isulu, katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga, watu watatu wanauguza majeraha ya risasi. Miongoni mwao ni Erick Msheti (19), ambaye alipigwa risasi kwenye nyonga, Victor Alvin Lodeki, aliyepigwa risasi mgongoni kabla ya risasi kutoka kwenye bega, na Joseph Mulama, aliyepigwa risasi tatu mkononi.

Msheti alisema walifika kwenye kikao cha ushirikishaji umma ambacho kilivurugika walipohisi maoni yao hayakuzingatiwa, ndipo polisi wakawafyatulia risasi.

“Hatutaondoka hapo. Hiyo ndiyo riziki yetu. Tunapata kidogo lakini kinatulisha. Hatutauza maisha yetu kwa fidia ya muda mfupi,” alisema Msheti, akidai anapata Sh12,000 hadi Sh20,000 kwa siku kupitia uchimbaji wa dhahabu.

Zaidi ya watu 63 walikamatwa kwenye msako usiku wa manane. Wazee, wanawake na watoto pia walijikuta mikononi mwa polisi.

Ijumaa asubuhi, mamia ya kina mama walijazana katika Kituo cha Polisi cha Kakamega wakitaka kuachiliwa kwa waume na watoto wao.

“Tunashangaa kwa nini polisi walivunja milango usiku kuchukua hata wale ambao hawakuhusika. Tumeleta vyeti vya kuzaliwa kuwaonyesha kwamba waliokamatwa ni watoto,” alisema Severina Muhandachi.

Kamanda wa Polisi wa eneo la Magharibi, Issa Mahmoud, alisema vijana waliokuwa na silaha butu ndio waliovuruga mkutano huo, na akadai shambulio hilo lilipangwa na kufadhiliwa na wanasiasa.

“Tumeweka ndani madiwani wawili waliokuwa wakigawa pesa,” alisema Mahmoud na kutambua madiwani hao kama Aketiye Liyai (Idakho South) na Ann Mulwale (mteule).

Kwa mujibu wa polisi, maafisa 21 walijeruhiwa na wawili bado wako hospitalini. Kituo kidogo cha polisi kilivamiwa na washambulizi wakajaribu kumpokonya bunduki afisa wa cheo cha Inspekta bunduki yake.

“Lengo lao lilikuwa kuingia kwenye ghala la silaha. Tuliwazuia,” alisema Mahmoud.

Mkuu huyo wa Polisi alidai kuwa mmoja wa waliouawa alikuwa na kesi ya mauaji inayoendelea, akihusishwa na kumuua mlinzi wa kampuni ya Shanta Gold miezi iliyopita.

“Kama hamkubaliani na mikutano ya ushirikishaji wa umma, kuna njia nyingine kama kuwasilisha malalamishi au kusimamisha shughuli kupitia mahakama ,si kutumia vurugu,” alisema Bw Mahmoud.

“Tayari tumemkamata mtu aliyempiga askari wa kike kichwani, na tunawafuata wengine wote waliohusika katika uhalifu wa jana. Tuna wahusika halisi baada ya kutambuliwa na polisi pamoja na umma,” akaongeza.

Alisema kuwa maafisa wa polisi watapiga kambi Isulu ili kuwakamata wale waliotoroka, akionya kuwa eneo hilo linaanza kugeuka kuwa “maskani ya wahuni na pombe haramu.”

Aidha, kuna timu ya makachero kutoka Nairobi ambayo imepelekwa kuchunguza chanzo halisi cha vurugu hizi na kuwatambua waliopanga na kuzitekeleza,” alisema.

Waandishi wa habari pia walijeruhiwa, na shule kadhaa kuvamiwa huku mali ya thamani ya Sh 2 milioni ikiharibiwa.

Haya si matukio ya kwanza. Migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa Isulu-Bushiangala na kampuni ya Shanta imekuwa ikiendelea kwa miaka.

Wenyeji wanapinga kutwaliwa kwa maeneo yenye madini na kampuni za kisasa wakihofia kufurushwa.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Faruk Machanje, alitaka serikali iache kutumia mabavu.

“Serikali izungumze na watu. Shanta ifunge ofisi zake Isulu hadi mgogoro utatuliwe,” alisema.

Naibu Gavana wa Kakamega, Ayub Savula, aliomba Nema kusitisha ushirikishaji wa umma hadi hali itulie.