Mwalimu wa JS ashtaki serikali kwa kuongeza muda wa kandarasi hadi miaka miwili
MZOZO unatokota katika sekta ya elimu baada ya mwalimu wa kibarua kuwasilisha kesi kortini akipinga uamuzi wa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kuongeza muda wa kandarasi za walimu vibarua wa Sekondari Msingi kutoka miezi 12 hadi 24.
Katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama ya Ajira na Leba jijini Nairobi, Nehemiah Kipkorir kupitia kampuni ya mawakili ya Mugeria, Lempaa & Kariuki, anataka maagizo kadhaa yatolewe kutangaza uamuzi huo kuwa kinyume cha Katiba na sheria.
Bw Kipkorir anataka mahakama ibatilishe uamuzi huo na kuilazimisha TSC iheshimu mkataba wa awali wa mwaka mmoja, akidai kuwa kuongeza muda huo bila mashauriano kunavunja haki za kimsingi kama mazingira bora ya kazi, usawa, heshima ya binadamu na utawala bora. Anasema kuongeza muda wa kandarasi za walimu hao vibarua hadi miezi 24 ni kinyume cha sheria, kinyume cha Katiba na ni hatua inayozidi mamlaka ya TSC.
“Hakukuwa na mashauriano na wadau, jambo linalokiuka Ibara ya 10 ya Katiba. TSC haina mamlaka ya kuajiri walimu vibarua nje ya majukumu yake ya kikatiba,” alisema Bw Kipkorir.
Pia anapinga dai kuwa hatua hiyo imetekelezwa kufuatia agizo la Rais, akisema ni kinyume cha Ibara ya 249 inayolinda tume huru dhidi ya kuingiliwa na serikali kuu.
Aidha, anataka amri itolewe ya kuajiri mara moja walimu wote waliokamilisha kikamilifu mwaka mmoja wakiwa vibarua kwa kandarasi za kudumu na za pensheni, pamoja na fidia kwa madai ya kukiukwa kwa haki zao.
Kesi hii imefufua mvutano upya kuhusu ajira katika sekta ya elimu, wakati ambapo walimu takribani 20,000 vibarua wameongezewa mikataba hadi mwaka 2026.
Naibu Mkurugenzi wa Elimu katika Tume ya Haki za Binadamu (KHRC), Cornelius Oduor, amelaumu serikali kwa kutumia mfumo wa kuajiri walimu wakufunzi akisema hauna msingi wa kisheria.
“Mahakama ilisema wazi kwamba kuwaajiri walimu waliohitimu kama vibarua ni kinyume cha sheria. Hawa ni walimu kamili waliostahili kuajiriwa—si wanafunzi. Kuwatumia kama vibarua ni kuendeleza ukosefu wa usawa,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Sekondari Msingi (KEJUSTA), James Odhiambo, alisema ni ukatili kufanya mwalimu kazi ya kibarua kwa muda wa miaka miwili.
“Hawa wanafanya kazi sawa na walimu wa kudumu lakini wanapokea mishahara duni bila posho zozote,” alisema Bw Odhiambo. Aliongeza kuwa Mahakama ya Leba tayari ilitangaza mfumo huo kuwa haramu na kuitaka serikali kuu kuufuta kabisa.