Mapigano yazuka upya mashariki mwa DRC saa chache baada ya Trump kusimamia mkataba
MAPIGANO yamezuka tena mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali, siku moja baada ya Rais wa Amerika Donald Trump kuwaalika viongozi wa DRC na Rwanda mjini Washington kusaini makubaliano ya amani yanayolenga kukomesha miongo kadhaa ya vita nchini humo.
Kila upande unalaumu mwingine kwa mapigano hayo mapya. Kundi la M23 lilidai katika taarifa kwamba watu 23 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya mabomu yaliyotekelezwa na jeshi la DRC.
Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka, alisema kwenye akaunti yake ya X kwamba vikosi vya Congo na washirika wao “wamelenga maeneo yenye watu wengi katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwa kutumia ndege za kivita, droni na mizinga mizito.”
Alidai pia kuwa mabomu mawili yaliyotokea Burundi Alhamisi jioni yalianguka karibu na mji wa Kamanyola na kuua watu wanne huku wawili wakijeruhiwa vibaya.
Kundi hilo lililoungwa mkono na Rwanda liliteka miji mikubwa miwili mashariki mwa DRC—Goma na Bukavu—mapema mwaka huu, na haliko chini ya masharti ya makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Amerika.
Afisa mmoja mkuu wa M23 ambaye hakutaka kutajwa jina aliambia Reuters kwamba waasi wamerejea kudhibiti mji wa Luberika na kuangusha droni ya jeshi la Congo.
Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la DRC alithibitisha kwa Reuters kuwa mapigano yanaendelea katika maeneo ya Kaziba, Katogota na Rurambo, jimbo la Kivu Kusini. “Kuna wakazi wanaotoroka maeneo ya Luvungi kwa sababu ya mabomu ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda. Wanayaangusha bila kujali,” alisema.
Jeshi na serikali ya Rwanda halikupatikana mara moja kutoa maoni.
Mapigano haya mapya yametokea siku moja baada ya Rais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda kuthibitisha tena kujitolea kwao kutekeleza makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Amerika mwezi Juni, yanayolenga kuleta utulivu na kufungua njia kwa uwekezaji mkubwa wa mataifa ya magharibi katika sekta ya madini.
“Tunamaliza vita vilivyoendelea kwa miongo kadhaa,” Trump alisema, akijipigia debe kama mpatanishi wa amani huku akitumia diplomasia kupanua masilahi ya biashara ya Amerika duniani.
Wachambuzi wanasema diplomasia ya Amerika ilizuia kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa DRC, lakini haikutatua chanzo cha mzozo.
Mapigano ya Ijumaa pia yalisababisha mamia kuhama makazi yao. Zaidi ya raia 700 wa DRC hasa wanawake na watoto—walivuka mpaka kuelekea Rwanda, afisa wa serikali ya wilaya ya Rusizi, Phanuel Sindayiheba, aliambia wanahabari. Alisema wakimbizi wanaendelea kuhifadhiwa kwa muda katika kituo cha mpito na kupatiwa chakula na mahitaji ya msingi.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wakimbizi wakielekea Rwanda kupitia mpaka wa Bugarama–Kamanyola, wengine wakiwa na mizigo na mifugo.
Kati ya Julai na Oktoba, zaidi ya watu 123,600 walifurushwa makwao DRC kutokana na mashambulizi ya makundi yenye silaha, mapigano, migogoro ya ardhi na majanga ya kiasili, kulingana na taarifa za hivi karibuni za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).