Uongozi dhaifu wa Oburu umeanza kuanikwa ODM
MIGAWANYIKO ya hivi punde katika ODM inatilia shaka uwezo wa Seneta wa Siaya Oburu Oginga wa kukiimarisha chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Mbali na uasi unaoendelezwa na viongozi wa chama hicho wenye umri mdogo, wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, kuhusiana na ushirikiano kati ya chama hicho na kile cha United Democratic Alliance (UDA) ndani ya Serikali Jumuishi, viongozi wengine sasa wanaonekana kufuatia nyayo za chipukizi hao.
Mnamo Jumanne, manaibu wa Dkt Oburu, Abdulswamad Sheriff Nassir, Simba Arati na Godffrey Osotsi pamoja na Mwenyekiti wa Kitaifa Glady Wanga, walikosa kuandamana naye kwa mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Hayo yalijiri baada ya Bi Wanga ambaye ni Gavana wa Homa Bay kumvua naibu wake Oyugi Magwanga wadhifa wa uwaziri kwa kuunga mkono mgombeaji huru Philip Aroko, katika uchaguzi mdogo wa Kasipul wiki jana.
Jumanne, Dkt Ruto aliwaalika Ikulu wabunge wapya waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM katika chaguzi ndogo zilizofanyika Novemba 27, 2025.
Wao ni Boyd Were ( Kasipul,Homa Bay), Moses Omondi (Ugunja, Siaya) na Magarini (Magarini, Kilifi).
Duru zimeiambia safu hii kwamba viongozi wakuu wa ODM, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Oduor Ong’wen, walikasirishwa na hatua ya Ikulu ya Rais kufeli kutuma mwaliko huo kupitia asasi za uongozi wa chama.
“Kwanza, wabunge hao wapya walipigiwa simu moja kwa moja. Kisha afisa mmoja alitumwa kwa Dkt Oburu kumshauri aandamane na wabunge hao wapya. Hii ni kinyume cha taratibu za chama chetu zinazohitaji kwamba mwaliko kama huo unapaswa kuwasilishwa kupitia sekritariati ya ODM,” akasema Mbunge mmoja anayehudumu muhula wa pili, aliyeomba tulibane jina lake.
Awali, saa za asubuhi, Dkt Oburu ODM alikuwa amewapokea rasmi wabunge hao wapya katika makao makuu ya chama hicho katika Jumba la Orange, Nairobi, katika hafla iliyohudhuriwa na Mbw Nassir, Osotsi, Arati, Bi Wanga miongoni mwa viongozi wengine wa chama hicho.
Lakini vinara hao wa ODM walidai walibanwa na shughuli nyingine ndipo wakafeli kufika Ikulu huku Bw Nassir ambaye ni Gavana wa Mombasa akiahidi kuwa mkutano mkubwa kati ya uongozi wa vyama vya UDA na ODM unapangwa baadaye mwezi huu ‘kuwakaribisha wabunge wetu wapya katika Serikali Jumuishi.’
Lakini afisa mmoja wa sekritariati ya ODM anamlaumu Dkt Oburu kwa kukubali kile alikitaja kama “njama ya Rais Ruto kudharua uongozi wa chama huku akipania kuwamiliki wabunge wetu wapya.”
“Inavunja moyo kwamba kiongozi wa chama anaonekana kukubali hatua kama hiyo saa chache baada ya kukariri kuwa ODM kitasalia chama huru katika ushirikiano wake na UDA chini ya Serikali Jumuishi,” akaeleza.
Hisia hizo zimejiri wiki ambayo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alidai kuwa Rais Ruto aliwahi kumfichulia kuhusu mpango wake wa “kumaliza” ODM.
Akiongea katika makao makuu ya chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Nairobi alipoongoza hafla ya kuwapokea rasmi madiwani watatu wapya waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho katika chaguzi ndogo wiki jana, Bw Gachagua alionya kwamba ushawishi wa ODM katika ngome yake ya Nairobi utaisha ikiendelea kushirikiana na Rais Ruto.
“Enyi Junet Mohamed na Gladys Wanga, mkiachilia ODM iende kwa Ruto, chama chenu kitaisha nguvu. Makali yenu yatasalia Luo Nyanza pekee,” akaonya.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati sasa anaonekana kukubaliana na kauli ya Bw Gachagua akisema Dkt Oburu na wenzake hawana ushawishi hitajika kuleta mshikamano ndani ya ODM.
“Sasa pendekezo la bintiye Raila Odinga, Winnie Odinga kwamba ODM inahitaji kuitisha Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake ili wachague viongozi wapya linaonekana kuwa na mashiko. Oburu hana moto na nguvu za kuimarisha ODM,” anaeleza.
Juzi, mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alitoa changamoto kwa uongozi wa sasa kutokubali “kumezwa na serikali”.
“Chama cha ODM kinakabiliwa na hatari ya kupoteza sifa zake za kupigania maslahi ya wanyonge na utawala wa kidemokrasia. Chama sasa kinageuzwa kuwa chombo cha kuisifia serikali,” akaeleza katika eneobunge lake.