Khalwale afunguka akidai hakuwahi kualikwa NEC ya UDA
BAADA ya kutemwa kama kiranja wa wengi katika seneti, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amefichua kuwa licha ya kuwa mwanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa la UDA, hakuwa akialikwa kwa mikutano ya chombo hicho cha maamuzi muhimu ya chama tawala.
Bw Khalwale alichagua Kakamega kufunguka mazito hayo siku mbili baada ya kuvuliwa wadhifa huo kwa kwenda kinyume na misimamo ya chama hasa kwa kupigia debe mgombeaji wa upinzani katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malava.
“Hata wanapofanya mikutano, mimi kama mwanachama wa NEC wa UDA, sikuwa nikiarifiwa wala kualikwa.”
Na alionekana kutumia wakazi wa Kakamega kama ngao baada ya masaibu yake akisema hiyo ni ishara wazi ya kutokushirikishwa kwao katika siasa za kitaifa, jambo ambalo alisema limekuwa chanzo cha changamoto zake kisiasa.
“Nimekataa kukubali kuwa Waluya hawahesabiwi. Ninasema mwaka 2027, wakati huu tutahesabiwa na tutatambulika. Nitahakikisha Kakamega inapata kiti kwenye meza ya kitaifa,” alisema Khalwale.
Katika uchaguzi mdogo wa Malava Novemba 26, Khalwale aliunga wazi mgombeaji wa upinzani, Seth Panyako, badala ya mgombeaji wa UDA, David Ndakwa, ambaye hatimaye alishinda kiti hicho kwa kura 21,564.
Uhusiano wa Khalwale na upinzani unaonekana kuimarika, kwani ameshirikiana waziwazi na viongozi wa Muungano wa Upinzani has kinara wa DAP-Kenya, Eugene Wamalwa.
Khalwale pia amehusishwa na chama chake cha United Patriotic Movement (UPM), ambacho kinachukuliwa kama chombo chake cha kisiasa kujiandaa kwa uchaguzi wa 2027.
Kwa mujibu wa Khalwale, mwelekeo wa UDA kuunga mkono Gavana Fernandez Barasa, umemfanya awe na uhakika kwamba chama hicho hakiwezi kumpa tiketi ya kugombea ugavana 2027.
Kwa wengi ufichuzi wake kwamba hakuwa akialikwa kwenye mikutano ya hadhi ya juu na hatimaye kuvuliwa wadhifa wake katika Seneti, Khalwale alijikaaga mwenyewe kwa vitendo vyake kinyume na misimamo ya chama tawala bila kufahamu UDA ina wenyewe.
Kwa sasa, Khalwale hana budi kuelekeza nguvu zake kisiasa kupitia UPM na kushirikiana na upinzani, akijiandaa kumenyania kiti cha ugavana Kakamega 2027.