Habari

Jumwa atangaza kutema UDA ahamia PAA ya Kingi

Na MAUREEN ONGALA December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, ameashiriwa kuwa atahama chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga na chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi.

Akizungumza na Taifa Jumapili, Bi Jumwa alisema kuwa ameamua kuunga mkono PAA, chama alichokitaja kuwa “cha nyumbani”.

“Nimetangaza msimamo wangu, na kilichosalia ni kujiunga rasmi na PAA na kuchukua wadhifa wa Naibu Kiongozi wa Chama,” alisema.

Katika uchaguzi wa 2022, Bi Jumwa alihusika katika kushawishi PAA kuingia katika muungano wa Kenya Kwanza baada ya kukihama chama cha Azimio la Umoja.

Alisema kabla hajafanya uamuzi wa kuondoka UDA, alifanya mashauriano ya kina na viongozi na wafuasi wake, akiongeza kuwa ni kawaida kwa wanasiasa kubadilisha vyama kila kipindi cha uchaguzi.

“Hata Rais Ruto amehama vyama mara kadhaa hadi akafika UDA. Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua pia aliwahi kuwa UDA na leo yuko DCP. Hivyo ndivyo siasa zilivyo,” alisema.

Bi Jumwa alisema Rais Ruto atasalia kuwa mgombeaji rais kuteteta kiti chake mwaka 2027, lakini PAA inalenga kushinda viti vyote vitano vya kuchaguliwa katika Kaunti ya Kilifi—Gavana, Seneta, Mwakilishi wa Wanawake, wabunge wa maeneo saba na madiwani 35.

Alisema uamuzi wake wa kuhama UDA ulisababishwa na “ukimya wa Rais” kuhusu chama chake wakati wa ziara zake Pwani.

“Hata Rais anapokuja Kilifi, hazungumzi kuhusu UDA. Mimi niseme nini? Nilimuunga kwa sababu ya upendo nilionao kwake, lakini inaonekana kama amesahau chama,” alisema.

Katika kampeni za 2022, Bi Jumwa alikuwa msitari wa mbele kupigia debe UDA, safari aliyosema haikuwa rahisi kutokana na upinzani mkali kutoka ODM.

Alisema ingawa Rais Ruto alipenda ODM “kwa sababu ya marehemu Raila Odinga,” haingewezekana kisiasa kuunga mkono chama hicho wakati huo.

Aidha, alitangaza kuwa yuko tayari kumkabili Gavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro (ODM), katika uchaguzi wa 2027 na kumuondoa mamlakani.

Tangu 2007, Kilifi imekuwa ngome ya ODM.

“Tunataka uamuzi wetu uwe mjadala wa kitaifa. Tuna Rais wetu na tunataka PAA ichukue viti vyote kutoka kwa Gavana hadi MCA,” alisema.

Hata hivyo, alithibitisha kuwa PAA itaingia makubaliano ya kisiasa na UDA katika serikali ijayo ya muungano.

“PAA iko Kenya Kwanza, ODM pia itashirikiana na Kenya Kwanza, na vyama vingine. Rais bila shaka atasalia William Ruto,” alisema.

Aliongeza kuwa si ajabu hata kuona DCP ikishirikiana na Ruto.

“Mradi tu kura za Rais Ruto ziko salama, mimi niko sawa.”

Alikana madai kwamba PAA ni chama cha Bw Kingi na anakitumia maslahi yake binafsi, akisema kila chama kina falsafa yake.

“Tuko PAA na tutaendelea kuwa humo. Tutaunga mkono na kubeba falsafa ya chama,” alisema.

Bi Jumwa alikiri kuwa ilikuwa vigumu kuuza UDA Pwani mwaka 2022 kwa sababu ya dhana kuwa ni chama cha jamii ya Wakalenjin.

“ODM ilitoka Nyanza na Gavana Gladys Wanga alikataza chama tawala kufanya kampeni huko, lakini alikuwa na ujasiri kuja Kilifi kuuza ODM. Hiyo haiwezekani,” alisema.

Bi Jumwa amewahi kuwa mwanachama wa ODM, chama alichotumia kushinda ubunge wa uwakilishi wa wanawake 2013 na ubunge wa Malindi 2017.