Kaeni rada, kutakuwa na mvua maeneo haya
Sehemu mbalimbali nchini zinatarajiwa kupata mvua katika kipindi cha siku tano zijazo, kwa mujibu wa utabiri mpya uliotolewa na Idara ya Hali ya Hewa Nchini.
Maeneo yatakayoathiriwa zaidi ni pamoja na Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Ukanda wa Ziwa Victoria, maeneo ya Kaskazini Mashariki na Kusini Mashariki. Haya ni licha ya sehemu nyingi za nchi kutarajiwa kubaki kavu na zenye jua.
Katika taarifa, idara hiyo ilibainisha kuwa mvua ya wastani hadi nzito itashuhudiwa kati ya Desemba 7 na Desemba 9. Nyanda za Juu Mashariki—ikiwemo kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi na hata Nairobi—zitaanza kuona mawingu asubuhi, mvua nyepesi baadaye, kisha vipindi vya jua kujitokeza.
Maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria kama vile Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii na Nyamira pia yanatarajiwa kupata mvua. Hali kama hiyo itajiri katika sehemu za Bonde la Ufa na Magharibi zikiwemo Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi.
Katika upande wa mashariki na kusini mashariki—hasa kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Taita Taveta na baadhi ya maeneo ya Tana River—manyunyu mepesi yanatarajiwa kuanzia Jumapili, Desemba 7, hadi Jumanne, Desemba 9, huku siku nyingine zikiendelea kuwa na mawingu.
Kwa upande wa Pwani, ikiwemo Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale, siku tano zijazo zinatarajiwa kuwa na jua na ukavu huku maeneo mengine ya nchi yakiendelea kupata hali sawa.
Idara ya hali ya hewa pia imetoa tahadhari ya baridi kali kwa wakazi wa Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu na Tharaka Nithi, ambapo halijoto ya usiku inaweza kushuka hadi nyuzi tano.
Wakati huohuo, maeneo ya Kaskazini Magharibi na mwambao wa Pwani yanatarajiwa kukumbwa na joto kali la mchana, likifikia hadi nyuzi 37 katika kaunti za kaskazini na nyuzi 33 katika kaunti za Pwani.