Habari

NTSA, NPS waanza ushirikiano kuzuia maafa ya ajali za barabarani msimu wa sherehe

Na CECIL ODONGO December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA ya Kitaifa ya Uchukuzi Barabarani (NTSA) na Tume ya Huduma za Polisi (NPS) zimesema zitashirikiana kuzuia maafa kwenye barabara nchini msimu huu wa sherehe.

NTSA na NPS zimezindua mpango wa usalama barabarani ambao utadumu kwa kwa miezi miwili na unalenga kuzuia maisha kupotea kupitia ajali za barabarani.

Kaimu Mkurugenzi wa NTSA Angele Wanjira alisema wanalenga kuhakikisha makosa ya kibinadamu na kiufundi yanayochangia ajali yanatokomezwa msimu huu sherehe za Krismasi na mwaka mpya zinajongea.

Kufanikisha usalama, ushirikiano wao na polisi utakuwa na umuhimu mkubwa kwenye oparesheni ya kuwanyaka wasiofuata sheria za trafiki.

Meneja wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA)wa eneo la South Rift John Parteroi akizungumza na abiria wakati wa msako wa matatu eneo la Salgaa, Desemba 4, 2025. Picha|Boniface Mwangi

“Tutakuwa tukiyakagua magari, kuendeleza mahamasisho ya umma na kushirikiana na abiria wenyewe kuhakikisha usalama wao,” akasema Bi Wanjira.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa kati ya Januari 1 na Oktoba 22, 2025 watu 3890 walikuwa wamefariki kwenye ajali ya barabarani na kupitisha idadi ya watu 3805 katika kipindi sawa na hicho mnamo 2024.

Kati ya wale ambao walikufa barabarani ni madereva 351, abiria 378, waendeshaji baiskeli 57 kisha waendeshaji wa pikipiki 1,000.

Bi Wanjira alisema NTSA itapanua mpango wa usalama barabarani ambapo abiria lazima wafunge mikanda ya usalama, magari yawe na vidhibiti mwendo na pia madereva wayaendeshe magari wakiwa hawajachoka.